SERIKALI YAFUTA STAND ZA MABASI KATIKATI YA JIJI LA ARUSHA KUPUNGUZA FOLENI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
ARUSHA — Serikali ya Mkoa wa Arusha imetangaza rasmi kufutwa kwa vituo vyote vya mabasi vilivyokuwa vikitumika katikati ya Jiji la Arusha kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria, hatua inayolenga kupunguza foleni sugu na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii ndani ya jiji hilo.
Tamko hilo limetolewa kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ambaye aliielekeza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha changamoto ya msongamano wa magari inashughulikiwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Katika kutekeleza agizo hilo, kikao maalum kimefanyika leo Jumatano, Januari 14, 2026, kikihusisha Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, TARURA, LATRA, TANROADS, Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Mipango Miji ya Jiji la Arusha. Kikao hicho kimeazimia kuwa mabasi yote ya abiria yatalazimika kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha (Arusha Main Bus Terminal) kuanzia safari zao zote.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Julius Kaaya, amesema utekelezaji wa agizo hilo unaanza mara moja, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni au mmiliki wa basi atakayekaidi maelekezo hayo.
“Hatutaruhusu tena mabasi kusimama au kutumia maeneo yasiyo rasmi katikati ya jiji. Lengo ni kupunguza msongamano na kurejesha nidhamu ya matumizi ya barabara,” amesema Mhandisi Kaaya.
Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji wa Jiji la Arusha, Bi. Doroth Absalom, ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za mipango miji, hairuhusiwi kabisa kwa kampuni za mabasi kutumia majengo ya makazi au biashara kama vituo vyao vya kupakia na kushusha abiria.
Amesisitiza kuwa kila basi linapaswa kuanzia na kumalizia safari zake katika Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha, huku akitoa onyo kali dhidi ya uoshaji holela wa mabasi pembezoni mwa barabara, kitendo kinachokiuka sheria na kuchangia uharibifu wa miundombinu pamoja na msongamano wa magari.
Hatua hii ya Serikali inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha usafiri wa umma, kuimarisha nidhamu ya matumizi ya barabara na kuifanya Arusha kuwa jiji safi, lenye mpangilio na rafiki kwa biashara na uwekezaji.




0 Comments