DC MKUDE AZINDUA MRADI WA KUKOPESHANA PIKIPIKI KWA WAENDESHA BODABODA ARUSHA,ATAKA UADILIFU WA FEDHA KWA VIONGOZI,AZANIA BENKI YACHOCHEA UCHUMI SEKTA YA MIKOPO.

 DC MKUDE ATAKA UADILIFU, NIDHAMU YA FEDHA KATIKA MIKOPO YA BODABODA ARUSHA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, amewataka viongozi wa bodaboda wilayani humo kusimamia mikopo ya pikipiki kwa uadilifu, uaminifu na nidhamu ya fedha, akisema misingi hiyo ndiyo nguzo ya kudumisha miradi ya kiuchumi na kuepusha mikopo kufa mapema.
Akizungumza Januari 14, 2026, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kukopeshana pikipiki wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Jiji la Arusha, Mkude alisema uzembe, ubadhirifu na kukiuka taratibu ndizo chanzo kikuu cha kushindwa kwa miradi mingi ya vijana.

Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa bodaboda kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria, akiwataka waendesha pikipiki wasiokuwa na leseni kujiorodhesha kwa makundi ili kupatiwa mafunzo ya usalama barabarani na kupewa leseni kwa utaratibu rafiki wa malipo ya awamu.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kuondoa urasimu usio wa lazima katika utoaji wa leseni, akisema lengo ni kuwahamasisha waendesha bodaboda wengi zaidi kujiunga na mfumo rasmi wa kisheria.

Mkude alionya kuwa operesheni dhidi ya pikipiki zinazokiuka sheria, ikiwemo kupiga mafataki, matumizi holela ya ‘trumpet’ na kufanya fujo mitaani, itaendelea bila kusita, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira ya bodaboda halali.

Mwenyekiti wa umoja wa bodaboda Jiji la Arusha, Shwahibu Hamisi amesema uongozi wa umoja huo umeingia makubaliano na kampuni ya uuzaji wa bodaboda aina ya TVS kuwakopesha wanachama wao pikipiki hizo na Kwa kuanzia wamekopesha pikipiki20.

" Pikipiki hizi ni kwamba tumetumia pesa tuliyochangiwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha milioni20 ambazo tumeamua kubadilisha matumizi kutoka kuanzisha ushirika na kuamua kukopeshana bodaboda," amesema.


Aidha Hamisi alimwomba DC Mkude kusaidia Wilaya ya Arusha kurejeshewa zaidi ya shilingi milioni 68 zinazodaiwa na Umoja wa Bodaboda wa Mkoa wa Arusha, fedha ambazo zinakusudiwa kutumika kununua pikipiki zaidi kwa ajili ya wanachama.


Mradi wa kukopeshana pikipiki unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuwawezesha kiuchumi waendesha bodaboda na kuboresha usalama barabarani katika Jiji la Arusha.




Kwa upande wake, mwakilishi wa Benki ya Azania Arusha,Paschal Siril ambaye ni meneja Mahusiano, alisema sekta ya bodaboda imekua kwa kasi na imekuwa chanzo muhimu cha ajira na uchumi, hivyo inapaswa kuaminiwa na kuungwa mkono na taasisi za fedha kwa mifumo rasmi na yenye uwajibikaji.

Kutokana na hilo, Benki ya Azania imeanzisha bidhaa maalum ya kifedha iitwayo JIKWAMUWE, inayolenga kuwahudumia waendesha bodaboda kwa mikopo ya mtu mmoja mmoja na vikundi, kwa masharti rafiki na uwazi unaoendana na uhalisia wa biashara hiyo.

Benki hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali na viongozi wa bodaboda kuhakikisha vijana wanapata mitaji ya kukuza biashara zao kwa nidhamu ya fedha, uadilifu na urejeshaji unaoaminika, kama mchango wa kukuza uchumi wa mkoa na taifa.



Naye mwakilishi wa Jeshi la Polisi ,Insp Kulewa Mziray alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kelele zisizofaa, matumizi ya ‘kerewa’ na uvunjaji wa sheria za usalama barabarani unaofanywa na baadhi ya waendesha pikipiki.

Amesema tayari operesheni zimefanyika katika maeneo mbalimbali, ambapo waendesha bodaboda waliokiuka sheria, wakiwemo wasio na leseni na wasiovaa helmeti, wamekamatwa na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.

Jeshi la Polisi limewataka waendesha bodaboda kushirikiana na mamlaka na viongozi wao, likisisitiza kuwa bodaboda ni ajira halali na muhimu, lakini lazima iendeshwe kwa kufuata sheria, kuheshimu jamii na kulinda usalama wa wananchi.







Ends...

Post a Comment

0 Comments