ALIYEKUWA NAIBU RAIS WA KENYA RIGATHI GACHAGUA AKIMBIA BAADA YA MABOMU YA MACHOZI KURINDIMA KANISANI, AMTUPIA LAWAMA RAIS RUTO
By Arushadigital – KENYA
ALIYEKUWA Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amelazimika kuondoka kwa haraka katika Kanisa la Wairima ACK lililopo Othaya, Kaunti ya Nyeri, baada ya mabomu ya machozi kurindima nje ya kanisa hilo, tukio lililosababisha hofu kubwa miongoni mwa waumini na kuvuruga ibada ya Jumapili asubuhi.
Gachagua, ambaye aliondolewa madarakani hivi karibuni baada ya kushtakiwa na Bunge la Kenya, alidai tukio hilo ni jaribio la kushambuliwa kisiasa, akimtuhumu moja kwa moja Rais wa Kenya William Ruto kuhusika na njama hiyo, ingawa hakuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha madai hayo mazito.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo kanisani hapo, vurugu zilianza mara baada ya ibada kuendelea, ambapo sauti za milipuko ya mabomu ya machozi zilisikika nje ya eneo la kanisa, hali iliyosababisha waumini kukimbia kwa hofu huku walinzi wa Gachagua wakimzingira na kumtoa kwa haraka kuelekea eneo salama.
Akizungumza kwa hasira muda mfupi baada ya tukio hilo, Gachagua alieleza kuwa matukio ya vitisho, ufuatiliaji na njama dhidi yake yamekuwa yakiongezeka tangu kuondolewa kwake madarakani, akidai kuna mkakati wa makusudi wa kumdhoofisha kisiasa na kumzuia kuwasiliana na wananchi, hasa katika eneo la Mlima Kenya.
“Hii ni ishara ya wazi kwamba kuna juhudi za kuninyamazisha. Hata nyumba ya Mungu haijaheshimiwa,” alikaririwa kusema Gachagua.
Tukio hilo limezua mjadala mpana nchini Kenya, huku wachambuzi wa siasa wakilitafsiri kama ishara ya mvutano mkubwa wa kisiasa unaoendelea kuongezeka kati ya uongozi wa sasa na waliokuwa washirika wake wa karibu, hali inayoweza kuathiri uthabiti wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa.
Hadi sasa, Serikali ya Kenya na Ikulu ya Rais hazijatoa tamko rasmi kujibu tuhuma zilizotolewa na Gachagua, wakati vyombo vya usalama vikidai vinafanya uchunguzi kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Tukio la Nyeri linaongeza orodha ya matukio tata yanayowahusisha wanasiasa wakuu nchini Kenya katika maeneo ya ibada, jambo linalozua maswali kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa na heshima ya maeneo ya dini katika mazingira ya mvutano wa kisiasa unaoendelea kushika kasi.
Kwa upande wake Gachagua amesema yuko salama nyumbani kwake Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri, eneo la Kati mwa Kenya, baada ya saa kadhaa za sintofahamu kuhusu aliko kufuatia tukio la Jumapili.
Hapo awali, Gachagua alidai kuwa "kikosi cha wauaji kikiungwa mkono na polisi wa eneo hilo," kilitekeleza agizo la Rais William Ruto, kwa kuvamia na kuvuruga ibada ya kanisa ambayo yeye na washirika wake walikuwa wakihudhuria.
Gachagua alisema kupitia mtandao wa X kuwa yeye na wafuasi wake walikwama ndani ya kanisa baada ya polisi kurusha mabomu ya machozi, akidai kuwa lilikuwa jaribio la mauaji. Alidai kuwa magari yake yaliteketezwa na kuiomba umma iwaombee.
“William Ruto ametuma kikosi cha wauaji kutuua ndani ya kanisa. Tumekwama tukishambuliwa kwa risasi na mabomu ya machozi,” aliandika.
Gachagua amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Ruto tangu alipoondolewa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye mwaka 2024.
Wasiwasi kuhusu usalama wake ilitanda mitandaoni baada ya ripoti kuwa maafisa wa usalama na watu wasiojulikana walivamia ibada ya Jumapili katika Kanisa la Wairima ACK, Othaya, Kaunti ya Nyeri, katika tukio ambalo lilisababisha Gachagua kuondolewa ghafla kanisani hapo na walinzi wake.




0 Comments