WAZIRI SHEMDOE AAGIZA TAARIFA YA KINA NDANI YA SIKU 14 KUHUSU MGOGORO WA UWEKEZAJI GEITA
Joseph Ngilisho- ArushaDigital,l- GEITA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Riziki Shemdoe, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhakikisha ndani ya siku 14 anawasilisha taarifa ya kina kuhusu mgogoro wa ardhi na uwekezaji unaomhusisha mwekezaji mmoja, anayedaiwa kubomoa miundombinu ya serikali na kuanzisha miradi bila kufuata taratibu za kisheria.
Agizo hilo limetolewa wakati wa kikao cha kazi kati ya Waziri Shemdoe na watumishi wa umma wa Mkoa wa Geita na Manispaa ya Geita, kufuatia kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii inayoonesha Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikilazimika kusimamisha shughuli za mwekezaji huyo, aliyekuwa ameanza ujenzi wa mradi katika eneo linalodaiwa kuwa ni viwanja vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Katoro.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa, mwekezaji huyo pia anatuhumiwa kuingilia na kuvuka mipaka ya ardhi ya Serikali ya Kijiji, hali iliyoibua mvutano mkali kati ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na viongozi wa kisiasa wa eneo hilo, wakiwemo Mbunge wa Jimbo la Katoro, Mhe. Kija Ntemi, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Geita, Mhe. Joseph Kasheku (Msukuma).
Mvutano huo ulifikia hatua ya juu zaidi baada ya Mbunge Joseph Kasheku (Msukuma) kutembelea eneo la mgogoro kwa lengo la kujiridhisha juu ya tuhuma za uvamizi wa ardhi ya umma.
Katika mazingira ambayo bado hayajawekwa wazi kikamilifu, ilibainika kutokea kwa tafrani kati ya Mbunge huyo na mwekezaji, hali iliyosababisha kurushiana makonde, tukio lililoshuhudiwa na baadhi ya wananchi na viongozi waliokuwapo eneo hilo.
Tukio hilo limezua mjadala mpana ndani na nje ya mkoa wa Geita, huku wadau mbalimbali wakitaka mgogoro huo ushughulikiwe kwa misingi ya kisheria na kitaasisi, ili kuepusha kuendelea kwa taharuki, vurugu na athari kwa amani ya jamii.
Akizungumza kwa msisitizo, Mhe. Shemdoe amesema serikali haitavumilia uvunjifu wa sheria, matumizi holela ya ardhi ya umma, wala uendeshaji wa miradi bila kufuata taratibu, na kusisitiza kuwa migogoro yote lazima itatuliwe kwa mujibu wa sheria bila kujali hadhi ya mhusika.
“Uwekezaji ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, lakini hauwezi kusimama juu ya kuvunja sheria au kupuuza mamlaka za serikali za mitaa,” amesema Waziri Shemdoe.
Ameelekeza taarifa inayosubiriwa iainishe kwa kina uhalali wa umiliki wa eneo husika, taratibu zilizofuatwa kabla ya ujenzi kuanza, nafasi ya halmashauri, kijiji na chama cha siasa, pamoja na mapendekezo ya hatua stahiki za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika endapo itabainika sheria zilikiukwa.
Waziri huyo pia amewataka viongozi wa kisiasa na kiutendaji kujizuia na vitendo vinavyoweza kuchochea mgawanyiko au kuvuruga amani, akisisitiza kuwa serikali inathamini uwekezaji halali unaozingatia sheria, mipango ya matumizi ya ardhi na maslahi ya wananchi.
Hatua ya TAMISEMI imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali kudhibiti migogoro ya ardhi, kulinda mali ya umma na kuimarisha utawala bora, hasa katika maeneo yanayokua kwa kasi ya kiuchumi kama Mkoa wa Geita.
ENDS..















0 Comments