DKT. LUKUMAY ACHAGULIWA KUONGOZA KAMATI YA BUNGE YA AFYA NA UKIMWI
Na Joseph Ngilisho- DODOMA
DODOMA — Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, hatua inayotafsiriwa kuwa imani kubwa ya Bunge kwa uwezo wake wa kitaaluma na kiuongozi katika sekta nyeti ya afya.
Uchaguzi wa Dkt. Lukumay umefanyika leo January 13,2026 jijini Dodoma wakati wa upangaji wa uongozi wa kamati za kudumu za Bunge, ambapo wabunge walimpa jukumu hilo kutokana na uzoefu wake mpana katika masuala ya afya, sera za jamii na utumishi wa umma.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Dkt. Lukumay alisema ataitumia nafasi hiyo kuimarisha usimamizi wa huduma za afya nchini, kuhimiza upatikanaji wa tiba bora kwa wananchi wote na kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi na mikakati jumuishi.
“Afya ya Mtanzania ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa. Kamati itashirikiana kwa karibu na Serikali, wadau wa maendeleo na jamii kuhakikisha sera na mipango ya afya inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi,” alisema Dkt. Lukumay.
Wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi pamoja na wadau mbalimbali wamepongeza uteuzi huo, wakisema ni heshima kwa jimbo hilo na mkoa wa Arusha kwa ujumla, huku wakieleza matumaini kuwa uongozi wake utaleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ina jukumu la kusimamia na kushauri utekelezaji wa sera, mipango na bajeti za sekta ya afya, ikiwemo kudhibiti maambukizi ya VVU/UKIMWI, kuboresha huduma za hospitali na vituo vya afya, pamoja na kuhakikisha haki ya afya kwa Watanzania wote inalindwa na kuendelezwa.
-Ends.

0 Comments