WAFANYABIASHARA ARUSHA WATISHIA MGOMO USIO NA KIKOMO MUDA WOWOTE,WADAI HALMASHAURI IMESHINDWA KUDHIBITI MACHINGA WANAOPANGA BIDHAA MBELE YA MADUKA YAO,WAMATAKA WAZIRI MWENYE DHAMANA

 WAFANYABIASHARA ARUSHA WATISHIA MGOMO, WAIOMBA SERIKALI KUDHIBITI MACHINGA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


WAFANYABIASHA wa Maduka jijini Arusha wametishia kuitisha mgomo na kufunga biashara zao kwa muda usiojulikana, iwapo Serikali itaendelea kulifumbia macho tatizo la wafanyabiashara wadogo maarufu kama mamachinga wanaopanga bidhaa zao mbele ya maduka yao, hali inayodaiwa kusababisha kushuka kwa mauzo na hasara kubwa kwa wafanyabiashara wanaolipa kodi.


Wakizungumza na vyombo vya habari jijini hapa, viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara wamesema hali hiyo imekuwa ikishamiri kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, licha ya wao kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Loken Adolf, alisema zaidi ya maduka 14,000 katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo yameathirika moja kwa moja na uwepo wa machinga wanaofanya biashara kiholela mbele ya maduka yao.


Alisema jumuiya hiyo imekuwa ikifanya vikao vingi na viongozi wa serikali za mitaa na wilaya kuhusu kadhia hiyo, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa hadi sasa, jambo linalowaacha wafanyabiashara wakiumia huku wakibebeshwa mzigo mkubwa wa kodi.




“Kumekuwa na taarifa zinazodai kuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, amewaruhusu mamachinga kupanga bidhaa zao popote. Sisi tunasema taarifa hizo si za kweli, na tunaomba Serikali ya Mkoa itoe ufafanuzi wa wazi kwa sababu hali hii inatuumiza sana wafanyabiashara wanaolipa kodi,” alisema Adolf.

Aliongeza kuwa tangu Agosti mwaka jana, wafanyabiashara wamekuwa wakikabiliwa na usumbufu mkubwa kutoka kwa mamachinga wanaowazunguka na kupora wateja wao, hali iliyosababisha baadhi ya maduka kushindwa kujiendesha kibiashara.

“Tumevumilia kwa muda mrefu, sasa imefika mwisho. Tuko tayari kufunga maduka yetu na kuacha kulipa kodi iwapo hatutapata suluhisho. Hatuwezi kuendelea kulipa kodi wakati hatuzalishi chochote,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Arusha, Dominick Mollel, alimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kuchukua hatua za haraka na kutoingiza siasa katika suala hilo, akisema wamachinga wamekuwa wakipanga bidhaa zao katikati ya barabara na mbele ya maduka, hali inayochangia msongamano na hatari kwa usalama.

Mollel alisema endapo tatizo hilo halitapatiwa ufumbuzi wa haraka, wafanyabiashara hawatasita kufunga maduka yao hadi Serikali itakapochukua hatua stahiki.

“Hakuna nchi inayoweza kuendeshwa bila walipakodi. Ikiwa machinga wataachwa wafanye biashara popote bila utaratibu, wafanyabiashara wa maduka watashindwa kulipa kodi, na uchumi wa jiji utaathirika,” alisema.

Aliitaka Serikali kuhakikisha masoko yaliyojengwa mahsusi kwa ajili ya wamachinga yanatumika ipasavyo kama yalivyokusudiwa, badala ya wafanyabiashara hao kuendelea kufanya shughuli zao kiholela mitaani.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Ahmed Nuru Jamal, alisema maduka yao yamevamiwa na mamachinga waliokimbia vizimba walivyopangiwa katika Soko la Kilombero, na sasa wanauza bidhaa zinazofanana na zile za wafanyabiashara wa maduka kwa kuzipanga mbele ya milango yao.

Alisema baadhi ya machinga wamekuwa wakivamia katikati ya barabara, huku wengine wakitokea mikoa na maeneo ya jirani ikiwemo Kilimanjaro, Babati, Karatu na Namanga, hali inayozidisha ugumu wa kudhibiti biashara hizo zisizo rasmi.

“Biashara zaidi ya maduka 14,000 jijini Arusha zimeathirika. Tunaiomba Serikali iingilie kati haraka kabla hali haijaharibika zaidi,” alisema Jamal.

Wafanyabiashara hao wamesisitiza kuwa hawapingi uwepo wa machinga, bali wanahitaji kuwepo kwa utaratibu rasmi, usawa wa kisheria na haki ya walipakodi, ili kuhakikisha shughuli za biashara zinafanyika kwa manufaa ya pande zote na kwa ustawi wa uchumi wa jiji la Arusha.



Bidhaa katikati ya barabara 




Post a Comment

0 Comments