Na Joseph Ngilisho – MONDULI
Katika kuendeleza jitihada za kukuza elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa Wilaya ya Monduli, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Isack Joseph Copriano, ameongoza zoezi la ugawaji wa vifaa muhimu vya shule kwa wanafunzi wenye uhitaji, ikiwa ni hatua ya vitendo ya kutimiza ahadi yake kwa wananchi.
Kwa niaba ya Mbunge huyo, Katibu wa Mbunge, Denis Morindati, alikabidhi vifaa hivyo kwa wanafunzi na wazazi wao katika hafla iliyofanyika nje ya Ofisi ya Mbunge, wilayani Monduli.
Vifaa vilivyotolewa vinatajwa kuwa ni msaada muhimu unaolenga kupunguza changamoto za mahitaji ya shule na kuongeza ari ya wanafunzi katika masomo.
Wananchi waliopokea msaada huo walieleza shukrani zao kwa Mbunge Mhe. Isack Joseph, wakisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha watoto wa Monduli wanapata elimu bora bila vikwazo.
“Kwa kweli kazi hii aliyofanya Mheshimiwa Mbunge hatutakaa tumsahau. Tunaendelea kumuombea Mungu ambariki na kumlinda. Tunaomba kwa kushirikiana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waendelee kutimiza ndoto ya kukuza elimu katika Wilaya ya Monduli,” alisema Stephano Maneno, mmoja wa wazazi walionufaika.
Kwa upande wao, wanafunzi waliopokea vifaa hivyo walionyesha furaha na shukrani, wakimuahidi Mbunge wao kusoma kwa bidii na kutumia fursa hiyo kama chachu ya kutimiza ndoto zao za maisha.
Zoezi hili ni la kwanza kufanyika tangu Mhe. Isack Joseph Copriano achaguliwe kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, ambapo katika awamu hii amekabidhi magodoro 150 na matranka 150.
Mbunge huyo ameahidi kuwa mpango huo utakuwa endelevu, akisisitiza azma yake ya kuhakikisha hakuna mtoto anayeshindwa kwenda shule au kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa vifaa vya shule.
Ends...








0 Comments