UHIFADHI SHIRIKISHI NGORONGORO: NCAA YAIMARISHA UHUSIANO NA JAMII, MIRADI YA MAJI YAPEWA KIPAUMBELE
By Arushadigtal-NGORONGORO
Jitihada za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika kujenga na kudumisha uhusiano imara na jamii zinazoishi ndani ya eneo la hifadhi zimeendelea kuzaa matunda, kupitia ziara za kikazi za Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, katika vijiji mbalimbali vya Tarafa ya Ngorongoro.
Katika mwendelezo wa ziara hizo, leo tarehe 20 Desemba, 2025, Kamishna Badru ametembelea Kata ya Enduleni, Wilaya ya Ngorongoro, kwa lengo la kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi pamoja na kusikiliza mahitaji yao ya msingi.
Akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya NCAA pamoja na Diwani wa Kata ya Enduleni, Mhe. Dkt. Elias Sakara Nagol, Kamishna Badru amesema ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka wa kuimarisha mahusiano ya karibu na jamii, sambamba na kukagua hali ya maboresho ya miundombinu ya maji inayotumika kwa matumizi ya wananchi, mifugo na wanyamapori.
Kamishna Badru ameeleza kuwa NCAA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika kata za Enduleni, Kakesio, Olbalbal na maeneo mengine ya Tarafa ya Ngorongoro, kama sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu za maji kwa jamii zinazoishi ndani ya hifadhi. Amesisitiza kuwa miradi hiyo ni uwekezaji mkubwa wa fedha za Serikali, hivyo ni wajibu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi, ulinzi na utunzaji wake ili idumu kwa muda mrefu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
“Ushiriki wa jamii ni nguzo muhimu ya uhifadhi endelevu. Tunapowekeza kwenye miradi ya kijamii kama maji, lengo letu ni kuboresha maisha ya wananchi huku tukihakikisha rasilimali za hifadhi zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Kamishna Badru.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Enduleni, Dkt. Elias Sakara Nagol, amempongeza Kamishna Badru na timu yake kwa kuendeleza uhusiano wa karibu na jamii kupitia ziara za mara kwa mara, kusikiliza changamoto za wananchi na kushirikiana nao katika masuala ya maendeleo ya kijamii.
Aliahidi kuwa wananchi wa Enduleni na maeneo jirani wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi shirikishi, kwa kulinda na kutunza rasilimali za hifadhi ya Ngorongoro kwa maslahi mapana ya taifa.
Ziara hiyo imeendelea kudhihirisha dhamira ya NCAA ya kujenga uhifadhi jumuishi unaoweka jamii kuwa sehemu ya suluhisho, si watazamaji, katika kulinda urithi wa asili wa Ngorongoro.
Ends..




0 Comments