TARURA ARUSHA YAIMARISHA USTAWI WA WATUMISHI KUPITIA MAFUNZO YA AFYA NA ZIARA YA KITALII NGORONGORO NA SERENGETI

TARURA Arusha Yaimarisha Ustawi wa Watumishi Kupitia Mafunzo ya Afya na Ziara za Kitalii

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


ARUSHA – Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Arusha imeendesha ziara maalum ya watumishi wake katika vivutio vikuu vya utalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti, sambamba na kutoa mafunzo ya namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo na changamoto za kiafya mahali pa kazi.



Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicholas Francis, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya taasisi, hususan lengo (A), linalolenga kudhibiti na kukabiliana na maambukizi ya VVU, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuboresha ustawi wa watumishi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mhandisi Nicholas alieleza kuwa semina iliyotolewa kwa watumishi ilijikita katika kuwapa elimu sahihi kuhusu hali halisi ya maambukizi ya VVU, njia za kujikinga, umuhimu wa kupima kwa hiari na kwa usiri, pamoja na kuondoa dhana potofu zinazokwamisha jitihada za kudhibiti na kuzuia kuenea kwa maambukizi hayo.

Aidha, washiriki walikumbushwa kuzingatia maadili ya kazi na maisha, kuchukua tahadhari binafsi na kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU katika mazingira ya kazi na katika maisha yao ya kila siku.

Vilevile, Meneja huyo aliwataka watumishi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia kutambua mapema hali zao za kiafya, kuongeza ari ya kufanya kazi na kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kuathiri ufanisi wao kazini.

Kwa mujibu wa TARURA Mkoa wa Arusha, mpango huo unaakisi dhamira ya taasisi katika kuweka mbele ustawi wa rasilimali watu kama nguzo muhimu ya maendeleo na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.












Ends..

Post a Comment

0 Comments