MKUU WA MKOA ARUSHA: “MBUNGE LUKUMAY NI MALI KWA WANANCHI”
Na Joseph Ngilisho – Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Makala, amemtaja Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, kuwa ni “mali kubwa” kwa wananchi wa jimbo hilo na Mkoa wa Arusha kwa ujumla, akisisitiza kuwa ni kiongozi mchapakazi, mzalendo wa dhati na mwenye mapenzi ya kweli kwa watu anaowaongoza.
Akizungumza katika kikao cha madiwani wa halmashauri ya Arusha alipotembelea halmashauri hiyo na kuwakutanisha viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi, CPA Makala alisema Dkt. Lukumay ni mfano wa mbunge anayeishi na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwatumikia Watanzania kwa upendo, uwajibikaji na kuwaletea maendeleo ya kweli.
“Dkt. Lukumay si mbunge wa maneno mengi bali ni wa vitendo. Ni msomi, mfuatiliaji na mchapakazi anayejua wajibu wake. Huyu ni mali kwa wananchi wa Arumeru Magharibi,” alisema CPA Makala.
Aliongeza kuwa sifa kuu ya mbunge huyo ni uwezo wake wa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa, huku akihakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kwa maslahi mapana ya wananchi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Dkt. Lukumay amekuwa mstari wa mbele kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kutembelea miradi mara kwa mara, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, umeme, elimu, afya na miundombinu.
“Ni kiongozi anayewapenda watu wake, anatembea nao, anawasikiliza na anachukua hatua. Haya ndiyo maono ya Rais Samia – uongozi wa huruma, uwajibikaji na maendeleo,” alisisitiza.
Kauli ya CPA Makala imepokelewa kwa shangwe na wananchi wa Arumeru Magharibi, ambao wamesema uongozi wa Dkt. Lukumay umeleta matumaini mapya na kasi ya maendeleo katika jimbo hilo, wakiahidi kuendelea kushirikiana naye kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.



0 Comments