NGORONGORO YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VITENDO VYA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO,SHIRIKA LA MEMUTE LAPONGEZWA

Na Joseph Ngilisho – NGORONGORO


WILAYA ya Ngorongoro mkoani Arusha imepiga hatua kubwa katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, hatua inayotajwa kuwa matokeo ya ushirikishwaji wa jamii, viongozi wa mila na juhudi za pamoja za taasisi za serikali na mashirika ya kijamii.


Hayo yamebainishwa leo desemba 10,2025 na Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo, Benezeth Bwigizo, wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, yanayofanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25. Katika Ngorongoro, maadhimisho hayo mwaka huu yamefanyika kijiji cha Losouto, kata ya Malon.

Bwigizo alisema mafunzo na elimu iliyotolewa kupitia mikusanyiko mbalimbali—ikiwahusisha viongozi wa mila, marika na makundi ya kijamii—imechangia pakubwa kupunguza ukatili uliokuwa umezoeleka kama sehemu ya utamaduni.


Alieleza kuwa vitendo vya ukatili vinavyojitokeza sana katika jamii hiyo ni pamoja na Ndoa za utotoni,Uke­ketaji,Ukatili wa majumbani (kipigo kwa wanawake) na Ubakaji.

Kwa mujibu wa Bwigizo, maboresho ya miundombinu ya elimu ikiwemo uongezekaji wa shule za bweni yamechangia kupunguza ndoa za utotoni na matukio ya ubakaji.

> “Miaka mitano iliyopita, kati ya wasichana 10, wasichana nane walikuwa wanaozeshwa. Kwa sasa, ni wasichana wanne tu kati ya 10. Hii ni hatua kubwa,” alisema.


Hata hivyo, alionya kuwa ukeketaji bado uko juu kwa asilimia 73, na juhudi zaidi zinahitajika ili kuukomesha kabisa.

Malengo ya 2030

Afisa huyo alisema wilaya imeweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, matukio ya ukatili yanapungua kwa kiwango kikubwa kupitia elimu, ufuatiliaji na utekelezaji wa sheria za nchi.

Pia alipongeza shirika la MIMUTIE ORGANIZATION ya jijini Arusha kwa mchango wake mkubwa katika kupigania haki za wanawake na watoto wilayani Ngorongoro, akisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu, uokoaji wa waathiriwa na kufuatilia kesi za ukatili.

Polisi Wataka Jamii Isikae Kimya


Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Lear Ncheyeki, alitoa rai kali kwa akina mama na watoto wanaofanyiwa ukatili kutokaa kimya, badala yake watoe taarifa kwa viongozi wa jamii na Jeshi la Polisi.

> “Kumkatili mtoto wa shule ni kosa la jinai. Wazazi tushirikiane kufichua matukio ya ukatili hasa majumbani dhidi ya wanawake. Tuwape watoto nafasi wasome na kutimiza ndoto zao,” alisema OCD Ncheyeki.


Aidha, aliitaka jamii ya wafugaji wa Kimasai kuanza kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, akisema ukame unaoendelea umeonyesha jinsi mifugo inavyopungua kwa kasi.

Wito kwa Jamii

Viongozi hao waliitaka jamii ya Ngorongoro kuendelea kushirikiana, kutoa taarifa za matukio ya ukatili na kufuatilia mienendo ya watoto ili kuwalinda dhidi ya vitendo vinavyowakatisha masomo na kuharibu maisha yao.






Ends...

Post a Comment

0 Comments