Na Joseph Ngilisho – NGORONGORO
MBUNGE AFANYA ZIARA NZITO YA UKAGUZI WA MIRADI YA MAJI, AHIDI MAGEUZI MAKUBWA TARAFANI LOLIONDO NA SALE
Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro ameendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa huduma endelevu za maji, baada ya kufanya ziara ya awali ya ukaguzi wa miradi mbalimbali katika Tarafa za Loliondo na Sale.
Ziara hiyo, ambayo ni sehemu ya mpango mpana wa kukabiliana na changamoto ya maji katika jimbo hilo, imempa Mbunge matumaini mapya kutokana na kasi ya utekelezaji wa miradi inayoendelea kujengwa na kuboreshwa katika maeneo kadhaa.
Mbunge huyo amesema kuwa kesho atakamilisha ukaguzi katika maeneo yaliyosalia ndani ya tarafa hizo, na tarehe 15 Desemba ataendelea na ziara katika Tarafa ya Ngorongoro, ikiwa ni mwendelezo wa usimamizi wake makini wa miradi ya maji.
Katika ziara ya leo, Mbunge ametembelea miradi ya Wasso, Loliondo, Sakala, Mugholo na Mageri—maarufu kama Mradi wa Vijiji 8—na kujionea maendeleo yaliyofikiwa pamoja na changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Mradi wa Wasso unaohudumia maeneo ya Wasso, Lopulun, Hospitali ya Wilaya, Lemishiri hadi Oldoinyowass unaendelea vizuri, ingawa bado kuna changamoto ya uharibifu wa mabomba katika laini ya Oldoinyowass.
Mbunge amesema atafika katika eneo hilo ili kujionea kwa karibu na kusaidia kuweka utaratibu wa kupata suluhisho la kudumu.
Kazi katika mradi wa Sakala zinatarajiwa kukamilika Jumatatu, na wananchi wataanza kupata maji Jumanne. Viongozi wa Kitongoji na Chama wametoa hakikisho hilo mbele ya Mbunge, na wananchi kuhamasishwa kuanza kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa maji.
Katika Kijiji cha Ng’arwa, Mbunge alikagua chanzo cha Emburbul chenye tangi kubwa la kusambaza maji kwenye Vijiji 8. Ujenzi umefikia asilimia 50, lakini umesimama kutokana na kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi.
Hata hivyo, jitihada za kuendelea na kazi zinaendelea kuimarishwa, licha ya umbali mrefu wa mabomba kuelekea Mageri, Mgongo, Magaiduru na maeneo
Katika Mugholo, mradi wa maji umefikia asilimia 85 baada ya kukamilika kwa tangi la lita 100,000 lililofadhiliwa kupitia mpango wa PfR. Kiasi cha shilingi milioni 50 kinahitajika kutandaza mabomba kwa wananchi, na Mbunge ameahidi kufuatilia kwa karibu hadi fedha zipatikane.
Wananchi wa Mageri wametoa maelezo ya kina kuhusu changamoto ya maji na maendeleo ya Mradi wa Vijiji 8. Mbunge amethibitisha kuwa Serikali imedhamiria kukamilisha mradi huu mapema iwezekanavyo.
Mazungumzo yake na Mkurugenzi wa AUWSA yameonyesha utayari mkubwa wa kusukuma kasi ya mradi ili ufikie ukamilishaji kabla ya Juni 2026.
Baada ya hapo, Mbunge alikagua matenki yaliyokamilika ambayo yanasubiri kupokea maji kutoka "Tanki Mama", hatua inayoashiria maandalizi mazuri ya usambazaji wa maji katika vijiji vinavyonufaika.
Katika eneo la Olorien, Mbunge alikagua mradi wa tanki lililokusudiwa kuhudumia cattle trough na cattle dip. Wananchi walilazimika kutumia maji ya bomba la dip kutokana na kituo chao maalumu cha kuchotea maji kutofanya kazi.
Mbunge ameagiza kituo cha DP kifunguliwe mara moja huku Mwenyekiti wa Kijiji akielekezwa kusimamia huduma hiyo wakati ukisubiriwa kupata msimamizi wa kudumu.
— Mwisho —











0 Comments