Mwanamke ajinyonga Rukwa, uchunguzi wa polisi unaendelea
By Arushadigital-RUKWA
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Joyce Mwasumbi, mkazi wa Kijiji cha Kanazi, wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amefariki dunia baada ya kujinyonga ndani ya chumba chake kwa kutumia kitenge, katika tukio lililotikisa wakazi wa kijiji hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanazi, Rudis Ulaya, amesema tukio hilo limetokea Desemba 24, mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi. Alisema marehemu, ambaye alikuwa mke wa Mchungaji wa Kanisa la EAGT katika kijiji hicho, Ibrahimu Mwaipopo, alibaki nyumbani wakati mumewe alipoondoka kwenda kanisani kufanya shughuli za kupalilia eneo la pembeni mwa jengo la kanisa.
“Baada ya muda, majirani walihisi kuna hali isiyo ya kawaida ndipo walipotoa taarifa. Ilipofanyika ukaguzi, ilibainika kuwa mwanamke huyo alikuwa amefariki dunia,” amesema Ulaya.
Ameongeza kuwa uongozi wa kijiji ulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambalo lilifika eneo la tukio na kuanza taratibu za uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo. Mwili wa marehemu umechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kulingana na taratibu za kisheria.
Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa familia, waumini wa kanisa hilo pamoja na wakazi wa Kijiji cha Kanazi, ambapo marehemu ameelezwa kuwa alikuwa mtu wa amani na mshikamano katika jamii.
Uongozi wa kijiji umewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama na pia kuwahimiza watu wenye changamoto za kisaikolojia au kifamilia kutafuta ushauri na msaada mapema ili kuepusha matukio kama hayo.
Jeshi la Polisi linatarajiwa kutoa taarifa zaidi pindi uchunguzi utakapokamilika.

0 Comments