MFANYABIASHARA AJITENGA NA TUHUMA ZA KISIASA: ASEMA ESTHER LUXURY COACH SI MALI YA WAZIRI MKUU
Na Arushadigital-MOSHI
MFANYABIASHARA na mwekezaji wa sekta ya usafiri wa abiria, Joseph Ngeleuya, mmiliki wa kampuni ya Esther Luxury Coach, amekanusha vikali taarifa zinazomhusisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, na umiliki wa kampuni hiyo, akizitaja madai hayo kuwa si ya kweli na yameleta madhara makubwa kwa biashara yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 27, 2025, katika Mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Ngeleuya amesema ameamua kujitokeza hadharani kutoa ufafanuzi wa kina na sahihi kufuatia taarifa zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, zikidai kuwa kampuni hiyo inamilikiwa au inahusishwa na viongozi wakuu wa kisiasa nchini.
“Nimewaita hapa leo kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa ukweli kuhusu taarifa potofu zinazohusu kampuni yangu ya usafirishaji, Esther Luxury Coach. Kumekuwapo madai yasiyo ya kweli yanayoihusisha kampuni hii na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba. Napenda kuweka wazi kuwa madai hayo hayana msingi wowote,” amesema Ngeleuya.
Ameeleza kuwa kutokana na tetesi hizo, kampuni yake imeathirika kwa kiwango kikubwa wakati wa machafuko yaliyojitokeza baada ya uchaguzi, ambapo waandamanaji waliivamia kampuni hiyo, kuchoma mabasi sita na kuharibu mali nyingine.
“Ninapenda kuwajulisha waandishi wa habari na Watanzania wote kuwa Esther Luxury Coach ni mali yangu binafsi na ya familia yangu. Haijihusishi kwa namna yoyote na kiongozi yeyote wa kisiasa au mtu mwingine yeyote nje ya familia yangu,” alisisitiza.
Ngeleuya amebainisha kuwa kampuni hiyo ina wanahisa wawili pekee, ambao ni yeye na mkewe, Neema Peter Thomas, na kwamba jina Esther lilichaguliwa kwa heshima ya mtoto wao wa kwanza, Esther Joseph Ngeleuya.
“Huo ndio uhalisia wa umiliki wa kampuni yetu. Ni biashara ya kifamilia iliyoanzishwa kwa juhudi na rasilimali zetu wenyewe,” ameongeza.
Akizungumzia athari za matukio hayo, mfanyabiashara huyo amesema maandamano ya kundi la Genz yaliyofanyika Oktoba 29, 2025, yamesababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa kampuni yake, inayokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 2.1, baada ya mabasi sita kuteketezwa kwa moto.
Kwa masikitiko, Ngeleuya ametoa wito kwa Watanzania kuacha kufanya maamuzi ya kuharibu mali za watu kwa misingi ya tetesi na taarifa zisizothibitishwa.
“Hasara tuliyoipata ni kubwa sana na inaumiza. Tunawaomba Watanzania wawe wavumilivu, wachunguze ukweli kabla ya kuchukua hatua zinazoweza kuwaumiza watu wasio na hatia,” amesema.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa yuko tayari kushirikiana na vyombo husika kuhakikisha ukweli unawekwa wazi na haki inatendeka.

0 Comments