MGOGORO WA KIFAMILIA WAKATISHA MAISHA YA MUME ,AAMUA KUJINYONGA BAADA YA MKE KUMWAMBIA AMLIPE MAHARI

 MSIBA: Mwanamume Ajinyonga Arusha, Mgogoro wa Ndoa Watajwa KuchangiaNa Arusha digital Arusha

MWANAUME mmoja anayefahamika kwa jina la Cleofasi Forentin Oiso (35), mkazi wa Mtaa wa Olkung’, Kata ya Terati, Jiji la Arusha, amefariki dunia baada ya kujinyonga katika makazi yake, tukio linalodaiwa kuhusishwa na mgogoro wa kifamilia uliokuwapo kati yake na mkewe.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka kwa majirani na watu wa karibu na familia hiyo, marehemu alikuwa ameishi na mkewe Anderika Kessy(32l kwa takribani miaka minane, wakiwa wamebarikiwa kupata watoto wawili. Chanzo cha mvutano huo kinatajwa kuwa ni suala la mahari, ambapo ilidaiwa kuwa mkewe alifungasha nguo zake akionesha nia ya kuondoka nyumbani hadi pale mahari itakapolipwa.

Hata hivyo, mke wa marehemu amekanusha vikali madai ya kutishia kuondoka, akieleza kuwa hakufungasha mizigo kwa nia ya kuvunja ndoa bali alimkumbusha mumewe kuhusu ahadi ya kulipa mahari, jambo ambalo, kwa maelezo yake, lilikuwa limejadiliwa mara kadhaa katika familia bila makubaliano ya mwisho.

Majirani waliokuwa karibu na marehemu wamesema kuwa siku moja kabla ya tukio, walizungumza naye na alionekana kuwa na huzuni, akieleza changamoto za kiuchumi alizokuwa akipitia. Kwa mujibu wao, marehemu aliwahi kusema kuwa angeweza kulipa mahari endapo hali yake ya kifedha ingekuwa nzuri, akionesha matumaini ya kuboresha maisha yake na familia kwa siku zijazo.

“Tulimwona akiwa na mawazo mengi. Alitaja ugumu wa maisha na alisisitiza kuwa hana nia mbaya, ila mambo hayakuwa sawa kiuchumi,” alisema mmoja wa majirani waliokataa kutajwa jina.

Tukio hilo limeibua sikitiko na majonzi makubwa kwa familia, hususan mke na watoto wa marehemu, pamoja na majirani na wakazi wa eneo hilo, ambao wameeleza kushangazwa na kifo hicho wakimtaja marehemu kuwa mtu mwenye mahusiano mema na jamii.

Viongozi wa mtaa wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa ziliwasilishwa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria na taratibu za uchunguzi, huku wakitoa wito kwa jamii kutafuta msaada wa ushauri nasaha na kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.

Tukio hili linakuja wakati jamii ikiendelea kukumbushwa umuhimu wa afya ya akili, ustawi wa familia, na mawasiliano yenye tija ndani ya ndoa, hasa katika nyakati za changamoto za kiuchumi, ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.

Post a Comment

0 Comments