MEYA IRANQHE AWATAKA MADIWANI KUWA WABUNIFU NA KUWASHIRIKISHA WADAU KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Meya wa Jiji la Arusha, Mhe. Maxmillian Matle Iranqhe, amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Jiji hilo kuimarisha ubunifu katika utendaji wao kwa kushirikisha wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto na kero zinazowakabili wananchi, hususan suala la miundombinu ya barabara.
Meya Iranqhe ametoa wito huo Desemba 27, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara katika Kata ya Terrat, jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Jiji kufuatilia na kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Meya alipokea taarifa kutoka kwa Diwani wa Kata ya Terrat ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Julius Ole Sakeyan, kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kutatua kero ya ubovu wa barabara katika kata hiyo. Taarifa hiyo ilieleza juhudi za kushirikisha mdau wa maendeleo,
Mchungaji Ruben Lereteti, ambaye ameridhia kutoa eneo la mlima wake wa Moram unaofahamika kama KwaruKwaru kwa ajili ya kuchimbwa kifusi (moram) kitakachotumika kukarabati barabara zilizoharibika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo inalenga kuhakikisha barabara katika Kata ya Terrat zinaboreshwa na kuwa zinazopitika wakati wote wa mwaka, hususan katika kipindi cha mvua ambapo changamoto ya usafiri imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Meya Iranqhe alipongeza ubunifu na ushirikiano uliooneshwa na uongozi wa kata hiyo pamoja na mdau wa maendeleo, akisisitiza kuwa huo ni mfano wa kuigwa na madiwani wengine wote wa Jiji la Arusha.
“Haya ni mafanikio yanayotokana na ubunifu na ushirikishwaji wa wadau. Nawahimiza madiwani wote kuweka mikakati shirikishi ili kutatua kero za wananchi badala ya kusubiri rasilimali za serikali pekee,” amesema Meya Iranqhe.
Aidha, Meya Iranqhe ameeleza kuwa Jiji la Arusha litaunga mkono jitihada hizo kwa kutoa vifaa kazi vitakavyowezesha uchimbaji wa moram katika mlima huo na usafirishaji wake hadi kwenye barabara zinazohitaji matengenezo.
Katika hatua nyingine, Meya huyo amebainisha dhamira ya dhati ya Jiji la Arusha katika kuimarisha miundombinu ya barabara kwa ujumla, akisisitiza kuwa suala hilo limepewa kipaumbele cha juu.
Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano wa viongozi mbalimbali wa Jiji hilo, wakiwemo Waheshimiwa Madiwani, Mkuu wa Wilaya, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, mikakati madhubuti imewekwa ili kuhakikisha barabara zote za Jiji la Arusha zinapitika wakati wote wa mwaka.
Meya Iranqhe amehitimisha kwa kuwahakikishia wananchi kuwa uongozi wa Jiji utaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya miundombinu ili kuboresha maisha na shughuli za kiuchumi za wakazi wa Jiji la Arusha.
Ends..



0 Comments