MBUNGE LUKUMAY ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA MADIWANI: “LEteni CHANGAMOTO, TUNAJENGA ARUMERU MPYA”
Na Joseph Ngilisho – Arumeru
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kasi na weledi kwa kubainisha changamoto zote zilizopo katika kata zao ili ziwasilishwe ofisini kwake kwa ajili ya utekelezaji wa haraka wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza leo Dec 2,2023 wakati wa uapisho wa madiwani wa Halmashauri ya Arusha dc, Lukumay alisema dhamira yake ni kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi ndani ya kipindi cha miaka mitano, na hivyo kila kiongozi anatakiwa kuongeza juhudi ili wananchi waanze kuona matokeo chanya mapema.
Aidha Lukumay alibainisha kuwa tayari ameanza kushughulikia maeneo korofi hususan barabara zinazokuwa na vumbi jingi wakati wa kiangazi na kutopitika msimu wa mvua, hali inayowapa wananchi usumbufu mkubwa.
> “Nimekutana na Waziri wa Ujenzi alipotembelea Arumeru na kumwomba kipande cha barabara kutoka Ngaramtoni Stendi hadi Hospitali ya Seliani kiwekwe lami. Ameupokea na kukubali ombi hilo, hivyo utekelezaji unaanza,” alisema.
Aliongeza kuwa mitambo ya ujenzi wa barabara tayari ipo katika halmashauri hiyo na kinachosubiriwa ni kuainishwa kwa maeneo ili kazi ianze mara moja.
Mbunge huyo alisema atashirikiana kwa karibu na TARURA pamoja na TANROADS kuhakikisha barabara zote za jimbo hilo zinajengwa kwa viwango vya changarawe na lami, ikiwemo kusukuma kuhakikisha mradi muhimu wa barabara ya Mianzini – Timbolo – Ngaramtoni unakamilika kwa wakati.
Akizungumzia changamoto ya umeme, Lukumay alisema tayari ameonana na Mkurugenzi wa REA, ambapo wamekubaliana kutembelea maeneo yenye changamoto ili kutathmini na kusambaza umeme mara moja.
Madiwani Kuongezewa Uwezo
Mbunge huyo alimwomba Mkurugenzi wa halmashauri kuandaa mafunzo maalumu kwa madiwani ili kuwaongezea uelewa wa majukumu yao na namna bora ya kuwatumikia wananchi.
Alisema hata kama halmashauri haina bajeti, yuko tayari kudhamini mafunzo hayo ili yafanyike mapema iwezekanavyo.
> “Madiwani wakijengewa uwezo wataweza kuibua vyanzo vipya vya mapato katika kata zao na kuongeza mapato ya halmashauri kutoka bilioni 6.9 hadi bilioni 10 ndani ya miaka mitano,” alisema.
Lukumay alitoa wito kwa madiwani wote kufanya kazi kwa umoja na kujikita katika kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo, akisisitiza kuwa maendeleo ya Arumeru yatafikiwa kupitia ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.
-ends...






0 Comments