ARUSHA LUTHERAN MEDICAL CENTER YAJIPANGA KUWA KITOVU CHA HUDUMA ZA MOYO KANDA YA KASKAZINI,WAGONJWA 500 WAPIMWA
Na Joseph Ngilisho – Arusha
SERIKALI imeendelea kupongezwa kwa kuweka sera rafiki zinazowezesha Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu na taasisi za kidini katika kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Miongoni mwa taasisi zinazotekeleza kwa vitendo dira hiyo ya Serikali ni Arusha Lutheran Medical Center,(ALMC) hospitali inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia Dayosisi ya Kaskazini Kati, chini ya uongozi wa Askofu,GODSON MOLLEL pamoja na uongozi wa kitaasisi.
Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za upasuaji na matibabu kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani.
Hatua kubwa ya kimkakati ilipigwa mwezi Novemba 2025, baada ya Arusha Lutheran Medical Center kuingia makubaliano rasmi ya ushirikiano wa muda wa miaka 20 na Taasisi ya Jakaya Kikwete Surgical Institute (JKCI).
Ushirikiano huo una malengo makuu mawili: kwanza, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na za uhakika za afya; pili, kuimarisha na kupanua wigo wa huduma zinazotolewa ndani ya hospitali hiyo.
Akizungumzia ushirikiano huo leo desemba 31,2025 , Mkurugenzi wa ALMC,Dkt Goodwill Kivuyo alieleza kuwa moja ya vipaumbele vikuu ni kuimarishwa kwa huduma za moyo, ambapo Arusha Lutheran Medical Center imelengwa kuwa kituo kamili cha uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (One Stop Center) kwa Kanda ya Kaskazini.
Mbali na huduma za moyo, hospitali hiyo pia itaendelea kuboresha huduma nyingine muhimu ikiwemo matibabu ya mifupa, upasuaji wa jumla, magonjwa ya ndani, huduma za watoto, maabara, famasia pamoja na huduma za mionzi (radiolojia).
Uboreshaji huo utaenda sambamba na uwekezaji mkubwa wa mitambo ya kisasa, ikiwemo CT Scan ya kisasa, MRI ya kisasa, pamoja na vifaa maalum vya Cath Lab kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Hatua hizi zote zinalenga kuinua viwango vya utoaji huduma za afya katika Arusha Lutheran Medical Center, ili kufikia na kuzidi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku zikilenga kupunguza gharama na adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.
Utekelezaji wa mpango huu tayari umeanza, na unatarajiwa kuingia kikamilifu kuanzia Januari 2026.
Hata hivyo, kupitia ushirikiano kati ya ALMC na JKCI, kambi maalum ya huduma za moyo tayari imeanza katika hospitali hiyo, ikitoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo kwa wananchi.
Kambi hiyo, iliyoanza wiki hii, inatarajiwa kuhitimishwa Jumatatu januari tano, ikiwa ni fursa adhimu kwa wananchi kupima afya ya mioyo yao na kupata matibabu ya awali bila gharama yoyote.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema wananchi takribani 500 wamepata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kupitia kambi maalum iliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD).
"Kambi hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya ufunguzi wa hospitali hiyo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa utoaji wa huduma za moyo kati yetu na Hospital ya ALMC"Alisema Dk Kisenge.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo ni wa ubia wa muda mrefu unaotarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka 20, ukiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa za moyo katika Kanda ya Kaskazini na Tanzania kwa ujumla.
Kutokana na fursa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Arusha Lutheran Medical Center ili kunufaika na huduma hizo, sambamba na kupata elimu ya afya itakayowasaidia kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Ends..









0 Comments