RC Makala Akabidhi Sh Bilioni 2.3 Fidia ya Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa AFCON Arusha
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
HATIMAYE Serikali imekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 kwa wananchi waliopisha ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa kisasa utakaotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Makabidhiano ya hundi hiyo yamefanyika nje ya eneo la ujenzi wa uwanja huo, katika Kata ya Olmoti, Jijini Arusha. Hafla hiyo imehudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi, viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa maendeleo, jambo lililoonesha uzito na umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Hafla hiyo imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makala, na kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, wataalamu kutoka sekta ya ardhi pamoja na wananchi wanufaika wa fidia hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Makala alisema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati unaenda sambamba na kulinda haki na maslahi ya wananchi. Alisisitiza kuwa malipo ya fidia ni haki ya msingi kwa mujibu wa sheria na yanapaswa kulipwa kwa wakati, kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria.
“Maendeleo hayawezi kusimama, lakini hayawezi pia kujengwa kwa kuwanyanyasa wananchi. Ndiyo maana leo Serikali inatekeleza wajibu wake kwa kuwakabidhi wananchi fidia yao baada ya kupisha ardhi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huu wa AFCON 2027,” alisema . Makala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia kwa kuleta mradi huo mkubwa wa kitaifa mkoani Arusha, akisema ujenzi wa uwanja huo ni wa kihistoria na una manufaa mapana kwa wananchi.
Mkude alisema mradi huo utachochea ukuaji wa uchumi kwa kufungua fursa za ajira kwa vijana, kukuza sekta ya michezo, kuimarisha utalii na kuongeza mzunguko wa fedha katika Mkoa na Jijini Arusha. Aidha, aliwashukuru wananchi waliopisha ardhi yao kwa kuonesha uzalendo, uvumilivu na ushirikiano mkubwa kwa Serikali.
Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa AFCON 2027 unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuiinua Tanzania katika sekta ya michezo barani Afrika, sambamba na kuharakisha maendeleo endelevu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Naye Afisa mipangomiji wa jiji la Arusha,Doroth Absalom alisema kuwa ,eneo lote la mradi huo linaukubwa wa hekari 83 ,ambapo wananchi 12 ndio wanalipwa fidia ambapo kati ya hao wananchi 7 walishalipwa na halmashauri ya jiji ambapo wengine 5 ndio wanalipwa na wizara ya utamaduni Sanaa na michezo .
Ends..














0 Comments