MWANAUME AKATWA UUME NA MKEWE USIKU WA MANANE ARUMERU
Na Joseph Ngilisho, Arumeru
Mwanaume mmoja mkazi wa Kitongoji cha Juhudi, Kijiji cha Olevolosi, kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru, amenusurika kifo baada ya kukatwa uume wake na mkewe katika tukio la kushtua lililotokea usiku wa kuamkia Novemba 19, majira ya saa saba usiku.
Baraka Melami (40), ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Selian Ngaramtoni, alikatwa sehemu zake za siri na mkewe, Anna Melami (30), akieleza kuwa tukio hilo lilifanyika wakati akiwa kitandani na mkewe baada ya kudhani kuwa walikuwa wanaanza tendo la ndoa.
“Nilidhani anataka kufanya tendo la ndoa…”
TANGAZO:KAMPUNI YA UTALII YA RIBRIS SAFARIS YATANGAZA OFFER
Akizungumza hospitalini, Baraka alisema mkewe alimsogelea kitandani kama kawaida, bila ishara yoyote ya ugomvi, na hilo lilimfanya amwamini.
> “Baada ya kupata hisia, ghafla alichomoa kisu alichokuwa amekificha na kukata kabisa sehemu zangu za siri. Aliondoa kabisa kisha akatupa uvunguni,” alisema kwa maumivu makali.
Baraka alieleza kuwa licha ya kujaribu kupiga kelele, hakusikika kwa sababu mkewe alikuwa tayari amefungulia redio kwa sauti ya juu kabla ya kufanya shambulio hilo, hali inayodhaniwa kuwa mbinu ya kuficha makelele.
Akiwa anatokwa damu nyingi, aliweza kutoka nje ya nyumba ndipo majirani waliposikia mayowe yake na kumkimbiza hospitalini kwa msaada wa dharura.
Aomba msaada wa matibabu
Kutokana na hali yake ambayo bado si ya kuridhisha, Baraka ameomba watanzania wenye moyo wa huruma kumsaidia kugharamia matibabu yake ambayo yanahitaji fedha nyingi.
Uongozi wa kijiji wathibitisha tukio
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Juhudi, Jonas Kisite, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya kupigiwa simu na majirani.
> “Ni kweli tukio limetokea. Tulihakikisha anapata msaada wa haraka na vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi kubaini chanzo chake,” alisema Kisite.
Hadi sasa, chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika rasmi, huku uchunguzi wa polisi ukiendelea.
-ends..


0 Comments