WALIOTAKA KUMTEKA MFANYABIASHARA TARIMO AKIWEMO ASKARI POLISI WAFUNGWA JELA MIAKA 7

VIJANA WANE WAHUKUMIWA MIAKA SABA JELA KWA JARIBIO LA UTEKAJI WA MFANYABIASHARA TARIMO

Na Arushadigital – Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni jijini Dar es Salaam, imewahukumu vijana wanne akiwemo askari wa Jeshi la Polisi, Fredrick Nsato (21), kifungo cha miaka saba jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, ambaye pia aliwaachia huru washtakiwa wawili — dereva wa teksi Nelson Msela (24) na Anitha Temba (27) — baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao bila kuacha shaka.



Washtakiwa waliohukumiwa ni:

Fredrick Nsato (21) — askari wa Jeshi la Polisi na mkazi wa Kibamba, Isaack Mwaifuani (29) — bondia na mkazi wa Kimara,Bato Twelve (32) — bondia mkazi wa Kimara Bonyokwa na Benk Mwakalebela (40) — wakala wa mabasi katika Stendi ya Magufuli.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rugemalira alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri, vielelezo, na utetezi wa washtakiwa, Mahakama imejiridhisha kuwa washtakiwa wanne kati ya sita walihusika moja kwa moja katika jaribio la utekaji wa Tarimo.

> “Mahakama imebaini bila kuacha shaka kuwa washtakiwa hawa wanne walishiriki katika jaribio la kumteka Deogratus Tarimo, ingawa tukio hilo halikufanikiwa. Kwa msingi huo, kila mmoja anahukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kujaribu kuteka,” alisema Hakimu Rugemalira.


Aidha, alifafanua kuwa awali washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na kosa la utekaji kamili, lakini ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kuwa Tarimo alitekwa, bali alitelekezwa eneo la tukio, hivyo kosa likabadilishwa kuwa kujaribu kuteka.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, washtakiwa waliomba kupunguziwa adhabu wakidai walitenda kosa hilo bila kujua, wakieleza kwamba askari Nsato aliwadanganya kuwa wanakwenda kumkamata mtuhumiwa katika eneo la Kiluvya Madukani, Kinondoni, mnamo Novemba 11, 2024.

Hata hivyo, Hakimu Rugemalira alisema hoja hiyo haina mashiko kisheria kwa kuwa kila mtu anawajibika binafsi kwa vitendo vyake, hasa pale vinapovunja sheria.

> “Haki inapaswa kuwa fundisho kwa wote — hakuna aliye juu ya sheria, iwe ni askari, bondia au mwananchi wa kawaida,” alisisitiza Hakimu Rugemalira kabla ya kutangaza hukumu hiyo.


Mwisho.


Post a Comment

0 Comments