RAMSEY AWAASA BODABODA KUTOSHRIKI MAANDAMANO, AWATAKA WAHAMASISHE KUPIGA KURA

RAMSEY AWAASA BODABODA KUTOSHRIKI MAANDAMANO, AWATAKA WAHAMASISHE KUPIGA KURA

Na Joseph Ngilisho, Arusha

 

Mwenyekiti wa Itikadi, Siasa, Mafunzo na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Saiburani Ramsey, amekutana na zaidi ya waendesha bodaboda 300 jijini Arusha na kuwasihi kutoshiriki maandamano yanayodaiwa kuratibiwa kupitia mitandao ya kijamii tarehe 29 Oktoba, akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kutumia siku hiyo kwa shughuli za maendeleo.


Akizungumza katika mkutano huo uliowakutanisha pia viongozi wa umoja wa bodaboda mkoani humo, Ramsey aliwahimiza vijana hao kutoshawishika kujiingiza kwenye maandamano ambayo, kwa maneno yake, “yanaweza kuhatarisha amani iliyopo nchini.”

> “Nimewaomba mjiepushe na maandamano yasiyo na tija. Tuitumie siku hiyo kwa jambo la msingi — kupiga kura. Hiyo ndiyo njia halali ya kikatiba ya kufanya maamuzi na kuleta mabadiliko ya kweli,” alisema Ramsey.


Ramsey alisisitiza kuwa badala ya kushiriki maandamano, waendesha bodaboda wanapaswa kutumia siku hiyo kuwahamasisha na kuwasafirisha wananchi kwenda vituoni kupiga kura, huku akiahidi kusaidia kulipia nauli kwa bodaboda watakaoshiriki kusaidia usafiri huo.

Aidha, Ramsey aliwataka waendesha bodaboda kuwa na shukrani kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa baadhi ya tozo zilizokuwa zikiwakandamiza sekta hiyo.

> “Kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, leseni ya bodaboda ilikuwa Sh. 70,000 lakini sasa ni Sh. 30,000. Faini ilipungua kutoka Sh. 30,000 hadi Sh. 10,000. Kodi ya pato ya Sh. 65,000 imeondolewa kabisa, na kodi ya maegesho kutoka Sh. 25,000 hadi Sh. 17,000,” alifafanua Ramsey.


Aliongeza kuwa mpango wa sasa wa serikali ni kuhakikisha waendesha bodaboda wanapata mikopo kupitia halmashauri zao baada ya uchaguzi, ili waweze kujiendeleza kiuchumi kupitia vikundi vyao vya ushirika.

Kwa upande wao, baadhi ya waendesha bodaboda walimpongeza Ramsey kwa hatua hiyo, wakiahidi kuunga mkono juhudi za serikali na kuepuka kushiriki maandamano yasiyo na faida kwa taifa.

> Juma Mollel, mmoja wa waendesha bodaboda kutoka eneo la Ngaramtoni, alisema:

“Kauli ya Ramsey imetugusa sana. Sisi kama vijana hatutaki kurudi nyuma katika mambo ya vurugu. Tutatumia pikipiki zetu kusafirisha wananchi kwenda kupiga kura kwa amani.”

> Naye John Maico mwendesha bodaboda wa Kituo cha Sakina, alisema:“Tunaona serikali ya Rais Samia inatujali. Kupunguza tozo na kutupatia fursa za mikopo ni jambo kubwa. Hatuwezi kupoteza muda kwenye maandamano — tutaendelea kulinda amani ya nchi yetu.”


Ramsey alihitimisha kwa kuwataka vijana hao kuendelea kuwa walinzi wa amani, kutumia fursa zilizotolewa na serikali, na kuonesha uzalendo kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kupiga kura kwa amani na utulivu.

Ends..

Post a Comment

0 Comments