TWARIQA ARUSHA WAKESHA KULIOMBEA AMANI TAIFA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29

TWARIQA WAONGOZA MAOMBI YA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBAR 29

Na Joseph Ngilisho– Arusha


Waumini wa Taasisi ya Kiislamu ya Twariqa kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, wakiwakilisha wenzao wa mikoa mingine nchini, wamefanya mkesha maalum wa maombi ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Dua hiyo ilifanyika katika Zawia Kuu, makao makuu ya taasisi hiyo jijini Arusha, na kuhudhuriwa na mamia ya waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.


Akiongoza dua hiyo, Kiongozi Mkuu wa Twariqa Tanzania, Sheikh Said Hamis Migire, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi, akibainisha kuwa amani ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote.

> “Amani ni kitu cha msingi. Ikiipotea ni vigumu kuirudisha. Tumeona mataifa mengi ya Afrika yaliyopoteza amani na sasa wanajuta. Tunawaomba Watanzania wajiepushe na vurugu na badala yake watumie njia halali kudai haki zao,” alisema Sheikh Migire.


Sheikh Migire aliongeza kuwa taasisi hiyo kama chombo cha kidini, imeona umuhimu wa kuombea taifa ili uchaguzi mkuu uwe wa utulivu, uwazi na wenye kuheshimika, huku akiwataka wananchi kuepuka wito wowote wa kuchochea ghasia au maandamano yasiyo na tija.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, Sheikh Haruna Hussein, aliwataka viongozi wote wa dini nchini kuungana kwa pamoja katika maombi ya kuombea amani, akisema jukumu la kuilinda nchi ni la kila Mtanzania.

> “Tunawaomba Watanzania wote, hasa vijana, kutoshiriki katika maandamano au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani. Badala yake, wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani, kwa sababu huo ndio msingi wa demokrasia ya kweli,” alisema Sheikh Hussein.


Naye Kiongozi wa Wanawake wa Twariqa Taifa, Bi Rehema Athumani, aliwataka vijana kutokubali kutumiwa kama vibaraka wa kuleta vurugu, akisisitiza kuwa athari za machafuko huwakumba zaidi wanawake na watoto.

> “Kila mara machafuko yakitokea, wanawake na watoto ndio wanaoumia zaidi. Hawana pa kukimbilia. Hatujawahi kuona vita ikileta maendeleo. Ndiyo maana tumeamua kuliombea taifa letu ili Mungu atuepushe na balaa,” alisema Bi Rehema.

 

Akizungumza baada ya dua hiyo, Kiongozi wa Msikiti wa Ngarenaro ambaye pia ni Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa Twariqa, Sheikh Hassan Kileo, alisema maombi hayo ni ujumbe wa amani kwa Watanzania wote, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

> “Tunatoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wananchi kwa ujumla kutanguliza amani. Tofauti za kisiasa zisiwe chanzo cha chuki wala vurugu. Kura ni sauti ya amani, hivyo kila mmoja ajitokeze kwa utulivu na kuchagua kwa hekima,” alisema Sheikh Kileo.


Dua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mfululizo wa maombi yanayoendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini, yakilenga kuhimiza amani, mshikamano na ushiriki wa amani katika Uchaguzi Mkuu ujao.




Ends..






Post a Comment

0 Comments