JENERALI MABEYO (MST) AWAVISHA VYEO MAKAMISHNA WAANDAMIZI WA UHIFADHI NGORONGORO, ASISITIZA UADILIFU NA KUCHAPA KAZI

 

JENERALI MABEYO (MST) AWAVISHA VYEO MAKAMISHNA WAANDAMIZI WA UHIFADHI NGORONGORO, ASISITIZA UADILIFU NA KUCHAPA KAZI

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu), amewavisha vyeo makamishna wasaidizi waandamizi wa uhifadhi wawili na kuwataka kuwa mfano wa uadilifu, uwajibikaji na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Waliovishwa vyeo hivyo ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Brown O. Shimwela, anayesimamia Idara ya Fedha, na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Dkt. Amani Makota, anayesimamia Idara ya TEHAMA na Takwimu. Wote wamemaliza kwa mafanikio mafunzo maalum ya Jeshi la Uhifadhi.

Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi vyeo hivyo, Jenerali Mabeyo aliwahimiza viongozi hao wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku wakishirikiana kwa karibu na menejimenti ya mamlaka hiyo kuboresha zaidi huduma na miundombinu ya utalii.

> “Tuboreshe huduma za wageni, ikiwemo miundombinu ya utalii na vivutio vya malikale kama Mapango ya Amboni na Kimondo cha Mbozi,” alisema Jenerali Mabeyo.

“Tujenge mazao mapya ya utalii, tuyatangaze na kuyaendeleza ili kuongeza mtawanyiko wa wageni na mchango wa sekta hii katika pato la Taifa. Uboreshaji wa miundombinu uende sambamba na kuimarisha mifumo ya TEHAMA kwa maendeleo ya Watanzania wote,” aliongeza.

Aidha, Jenerali Mabeyo ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi Mstaafu, alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kushirikiana na watumishi wengine wa Ngorongoro katika kulinda rasilimali za Taifa, kuboresha huduma kwa wateja na kuhakikisha maeneo ya kihistoria na malikale yanayotunzwa na mamlaka hiyo yanachangia ipasavyo katika uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Bw. Abdul-Razaq Badru, alisema ujio wa makamishna hao wapya unaongeza nguvu kazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya mamlaka, yakiwemo uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

> “Utalii ni sekta kinara katika kuchochea uchumi wa nchi. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kushirikiana na wadau wa utalii kubuni na kutangaza mazao mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na pato la Taifa,” alisema Badru.


Sherehe hiyo ya uvishaji vyeo imefanyika katika ofisi kuu za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha nidhamu, ufanisi na uwajibikaji katika Jeshi la Uhifadhi nchini.




Ends....

Post a Comment

0 Comments