SERIKALI YAPANDISHA MSHAHARA KIMA CHA CHINI SEKTA BINAFSI

 By Arushadigital 


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) imetangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi, ambapo sasa kitakuwa Sh. 358,322, kutoka Sh. 275,060, ikiongezeka kwa asilimia 33.4.


Ongezeko hilo litaanza kutumika rasmi kuanzia Januari 1, 2026. Hii inakuja ikifuata ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma uliofanyika mwaka huu, ambapo mshahara wa chini zaidi wa umma ulipandishwa kutoka Sh. 370,000 hadi Sh. 500,000, sawa na ongezeko la asilimia 35.1


Alisema lengo ni kuimarisha ustawi wa wafanyakazi. Tangazo hilo lilitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa Mei mwaka huu mkoani Singida, katika viwanja vya Bombadia.


Akitangaza kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi leo Ijumaa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema ongezeko hilo ni takwa la kisheria. Amesema kuwa tangazo la mwisho lilikuwa mwaka 2022, na kwa mujibu wa sheria, kila baada ya miaka mitatu lazima kufanyike mapitio ya kima cha chini cha mshahara.


“Nitoe rai kwa waajiri wote wa sekta binafsi kuzingatia na kutekeleza kima hiki kipya cha mshahara kwa kuwa ni takwa la kisheria. Ofisi yangu haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza amri hii kwa makusudi,” amesema Waziri Kikwete.

Aidha, ameongeza kuwa ofisi yake itaendelea kufuatilia utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi, pamoja na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha kima cha chini cha mshahara kinatekelezwa kikamilifu.



Post a Comment

0 Comments