RC MAKALLA AANZA KUTEMA CHECHE AWAONYA “TATU MZUKA” WANAOPORA WANANCHI ARUSHA ,ATOA AGIZO ZITO KWA RPC MASEJO NA OCD MATAGI KUWALEA WAHALIFU.


RC MAKALLA AWAONYA “TATU MZUKA” WANAOPORA WANANCHI ARUSHA
Awataka waache uhalifu, watafute kazi halali
Na Arushadigital – Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ametoa onyo kali kwa vijana wanaotumia pikipiki kufanya vitendo vya uhalifu, maarufu kama Tatu Mzuka, akiwataka kuacha mara moja tabia hiyo na badala yake watafute kazi halali za kujipatia kipato.

Aidha, CPA Makalla amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha  na Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo, kuhakikisha wanachukua hatua kali dhidi ya vijana wanaotumia pikipiki kwa uhalifu, ili kudhibiti matukio hayo na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani na utulivu.

CPA Makalla alitoa onyo hilo leo, Oktoba 13, 2025, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa wa Arusha iliyopo katika kata ya Muriet, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ongezeko la matukio ya uporaji yanayofanywa na vijana hao.

“Tatu Mzuka popote walipo, natoa onyo kuachana na uhalifu wa kutumia pikipiki. Nasema wasinichokoze, nitakula nao sahani moja. Mkoa huu lazima uwe salama. Nikiwa Mkuu wa Mkoa, ni marufuku Tatu Mzuka kufanya uhalifu Arusha. Nawaonya, tafuteni kazi nyingine halali,” alisema CPA Makalla kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii na mikutano ya kimataifa, hivyo unapaswa kuwa salama na rafiki kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

“Arusha ina wageni wengi, kila mmoja lazima awe mlinzi wa usalama wa eneo lake. Tusikubali wachache wachafue jina la mkoa wetu,” alisisitiza.

Aidha, CPA Makalla amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha anachukua hatua kali dhidi ya vijana wanaotumia pikipiki kwa uhalifu, ili kudhibiti matukio hayo na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani na utulivu.

Amesema serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuvuruga amani, akibainisha kuwa usalama wa wananchi ni kipaumbele chake namba moja tangu aingie madarakani.

Mkuu huyo wa mkoa amehitimisha kwa kuwataka viongozi wa wilaya zote za Arusha, ikiwemo Jiji la Arusha, Arusha DC, Karatu, Monduli, Longido na Ngorongoro, kuendelea kuimarisha ulinzi na kushirikiana na vyombo vya dola kukomesha mtandao wa Tatu Mzuka unaowasumbua wananchi.


Mwisho
(Arushadigital – Habari mpya za kila siku Hapa Nyumbani)

Post a Comment

0 Comments