By Arushadigital
Pingamizi lililowekwa siku ya Ijumaa na Jamhuri kuhusiana na maombi ya mshtakiwa, Tundu Lissu anayejitetea mwenyewe kwenye kesi ya uhaini inayomkabili la kutaka kielelezo cha maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili limepingwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam mapema leo, Jumatatu Oktoba 13.2025 katika “uamuzi mdogo” uliotolewa.
Pingamizi hilo lilitokana na mshtakiwa ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo kuomba kielelezo D1 (maelezo ya maandishi ya shahidi wa pili wa Jamhuri Inspekta wa Jeshi la Polisi John Kaaya aliyoandika akiwa kwenye Kituo cha Polisi) cha PW2 ambaye ndiye shahidi, upande wa Jamhuri ulipinga kielelezo hicho kupokelewa Mahakamani hapo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mshtakiwa hajazingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria pale mshtakiwa anapotaka kumuhoji shahidi kuhusu maelezo aliyotoa hapo awali
Katika uamuzi wake, jopo la Majaji watatu (3) wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru wamesema mshtakiwa amefuata taratibu zote zinazohitajika kisheria katika kuomba kielelezo hicho kupokelewa Mahakamani
Wamesema kwa mujibu wa taratibu za kisheria panapotokea mazingira ya aina hiyo kuna hatua tatu (3) za kufuatwa, ikiwemo shahidi kusomewa maelezo yake, mshtakiwa kubainisha maeneo anayoona yana 'kasoro' kwa ulinganifu ili ayafanyie dodoso ambapo kwa muktadha wa kesi hiyo Mahakama imeona kuwa mshtakiwa alibainisha maeneo 45, na mwisho ni kumuhoji mshtakiwa endapo yuko tayari kielelezo hicho kipokelewe Mahakamani na kitumike kama sehemu ya ushahidi wake, hatua ambazo zote zilifuatwa
Kufutia maamuzi hayo ya Mahakama, sasa kielelezo hicho (D1) kinakuwa cha kwanza cha mshtakiwa Tundu Lissu kuwasilishwa Mahakamani hapo, na sasa kesi hiyo inaendelea ambapo mshtakiwa anaendelea kumuhoji maswali ya dodoso
-Ends

0 Comments