NSSF YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA KISHINDO ARUSHA ,THAMANI YA MFUKO YAPAA NA KUFIKIA TRILION 9.9

 NSSF YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA MAFANIKIO MAKUBWA YA KIFEDHA

Na Joseph Ngilisho,ARUSHA


MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja jijini Arusha kwa kishindo, huku ukitangaza mafanikio makubwa ya kifedha yaliyoupandisha mfuko huo kwa ongezeko la thamani la Shilingi trilioni 1.3, sawa na asilimia 19 katika kipindi cha mwaka mmoja pekee.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo Oktoba 6,2025 jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, John Masha Mshomba, hadi kufikia Juni 30, 2025, thamani ya mfuko imefikia Sh trilioni 9.9, ikilinganishwa na Sh trilioni 8.3 zilizorekodiwa Juni 30, 2024.

>

“Huu ni ushahidi wa wazi kwamba tunasonga mbele kwa kasi na mafanikio haya yanakwenda sambamba na utekelezaji wa malengo tuliyojipangia. Tumejenga msingi imara wa uaminifu, uwazi na ushirikiano kati ya waajiri, wafanyakazi na NSSF,” alisema Mshomba.


Akizungumzia maendeleo ya mfuko katika kipindi cha miaka minne tangu Machi 2021, Mshomba alisema ukuaji huo ni wa kihistoria.

>

“Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, thamani ya mfuko ilikuwa Sh trilioni 4.8, leo hii tumeifikisha hadi Sh trilioni 9.9 — sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100. Hii ni ishara ya uthabiti, usimamizi bora na imani ya wanachama wetu,” alifafanua.


Alisema, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa muda mrefu, NSSF imejipanga kufikia thamani ya Sh trilioni 11.5 ifikapo Juni 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya malengo ya kitaifa ya kukuza uwekezaji na hifadhi ya jamii kwa Watanzania wote.


Katika hafla ya maadhimisho hayo iliyofanyika katika jengo la Mafao House, jijini Arusha, na kuhudhuriwa na wanachama, waajiri, wastaafu na wachangiaji binafsi, Mshomba alisema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwashukuru wateja na wanachama kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio ya NSSF.

>

“Tunasherehekea mafanikio haya pamoja na wateja wetu. Kama ishara ya shukrani, NSSF imetoa zawadi mbalimbali zikiwemo majiko 100 ya gesi kwa wanachama, tukiiunga mkono serikali katika kampeni



ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda mazingira,” alisema.


Aliongeza kuwa, NSSF imekuwa ikiboresha huduma zake kila mwaka, na kwa sasa asilimia 97 ya huduma zote zinatolewa kwa njia ya kidigitali, hatua ambayo imepunguza usumbufu kwa wateja na kuongeza uwazi katika utendaji.

>

“Lengo letu ni kufikia asilimia 100 ya utoaji wa huduma kidigitali kabla ya mwaka huu kuisha. Huduma hizi zimeleta urahisi kwa wanachama kupata taarifa za mafao, michango na huduma nyingine bila kufika ofisini,” alieleza Mshomba.


Aidha, alitoa rai kwa wafanyakazi wote wa NSSF kuendelea kujituma zaidi ili kufikia malengo ya mfuko huo, sambamba na kuendelea kuwafikia wananchi walio jiajiri ili nao waweze kujiunga na kunufaika na huduma za hifadhi ya jamii ikiwemo matibabu na mafao ya uzeeni.

>

“Tunapanua wigo wa hifadhi ya jamii. Tunataka kila Mtanzania mwenye kipato, awe wa sekta rasmi au isiyo rasmi, awe sehemu ya NSSF,” alisema.


Kwa upande wao, baadhi ya wanachama walionufaika na huduma ya matibabu kupitia NSSF waliipongeza taasisi hiyo kwa huduma bora na kwa kuendelea kuboresha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya Watanzania.

Bi. Rehema Mollel, mkazi wa Ngaramtoni na mchangiaji wa muda mrefu wa NSSF, alisema huduma ya matibabu imekuwa msaada mkubwa kwake na familia yake.

>

“Nililazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili, lakini gharama zote zilitolewa na NSSF. Hii imenisaidia sana na imeniondolea mzigo mkubwa wa kifedha. Nawashukuru kwa huduma nzuri na haraka wanazotoa,” alisema.


Naye Bw. Elias Kaaya, dereva kutoka kampuni binafsi jijini Arusha, alisema amekuwa akinufaika na huduma za matibabu pamoja na mafao ya wazazi wake kupitia NSSF.

>

“NSSF imekuwa kimbilio letu sisi wafanyakazi. Hata ukiumwa, unapata huduma bora bila usumbufu. Wameboresha sana huduma kwa njia ya kidigitali na sasa kila kitu ni rahisi,” alisema.


Wachangiaji hao waliitaka NSSF kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, hasa wale wa maeneo ya vijijini, ili watanzania wengi zaidi wanufaike na hifadhi ya jamii.

Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa burudani, mijadala ya elimu kwa wateja na utoaji wa zawadi, huku wadau wakipongeza uongozi wa NSSF kwa ufanisi, uwazi na ubunifu unaoendelea kuuboresha mfuko huo wa taifa.










Ends..

Post a Comment

0 Comments