MSIMAMIZI WA UCHAGUZI ARUSHA APULIZA KIPYENGA,WENYE LESENI KURUHUSIWA KUPIGA KURA – UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025

WENYE LESENI KURUHUSIWA KUPIGA KURA – UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025

Na Joseph Ngilisho, Arusha


Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Arusha Mjini ,Shaban Manyama ametangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, kwa mujibu wa Kifungu cha 69(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, vituo vyote vilivyotumika wakati wa uandikishaji wa wapiga kura ndivyo vitakavyotumika pia katika upigaji kura siku ya uchaguzi. Vituo hivyo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

Kwa upande wa wapiga kura walioko magerezani, vituo vyao vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 9:00 alasiri, kuhakikisha kila mpiga kura anapata haki yake ya kikatiba.

Msimamizi huyo wa Uchaguzi amesema kuwa tayari taarifa muhimu zimebandikwa katika kila kituo cha kupigia kura, zikiwemo,Mfano wa karatasi ya kura yenye majina, picha na nembo za vyama vya wagombea wa nafasi za Rais, Wabunge na Madiwani,Orodha ya wapiga kura walioandikishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),Orodha ya wapiga kura waliopangiwa kupiga kura ya Rais pekee.


Wananchi wote wametakiwa kupitia orodha hizo mapema ili kujiridhisha kuwa majina yao yapo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kubaini vituo vyao sahihi kabla ya siku ya uchaguzi.

Katika siku ya uchaguzi, kila mpiga kura anatakiwa kufika kituoni na kadi yake ya mpiga kura.

Hata hivyo, wale waliopoteza kadi zao lakini wamesajiliwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wataruhusiwa kupiga kura endapo watakuwa na kitambulisho mbadala kama,Leseni ya udereva,Pasi ya kusafiria, auKitambulisho cha Taifa (NIDA).

Ni sharti majina yaliyomo kwenye kitambulisho mbadala yawe yanalingana na yaliyoko kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kuruhusiwa kupiga kura.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Arusha Mjini amewataka wananchi kujipanga mapema, kuthibitisha vituo vyao vya kupigia kura, na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kutumia haki yao ya kidemokrasia.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza amani, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akibainisha kuwa Tume inatarajia uchaguzi wa uwazi, utulivu na haki kwa pande zote.

> “Tunawahimiza wananchi wote wa Arusha Mjini wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi, wachague viongozi wanaowaamini kwa amani na utulivu. Uchaguzi huu ni wa Watanzania wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kushiriki na kulinda amani ya taifa letu,” alisema Msimamizi wa Uchaguzi huyo.




Mwisho

#ArushaDigital | Habari za Uchaguzi Mkuu 2025


Post a Comment

0 Comments