Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
WAHITIMU wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Nakido iliyopo jijini Arusha wametakiwa kuyaishi kwa vitendo yale mema waliyojifunza wakiwa shuleni, hususan elimu ya Amali inayowaandaa kuwa wabunifu, wajasiriamali na wachapa kazi.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 10 ya shule hiyo, Mwalimu Ally Kiluvia, ambaye alimwakilisha Afisa Elimu wa Jiji la Arusha, aliipongeza shule hiyo kwa kutekeleza kwa ufanisi mtaala mpya ulioboreshwa wa mwaka 2023, unaolenga kutoa elimu ya vitendo kuanzia madarasa ya awali hadi sekondari.
Kiluvia alisema mtaala huo umekuwa chachu ya maendeleo ya elimu nchini, akibainisha kuwa wanafunzi wa Nakido wameonyesha ubunifu mkubwa katika masuala ya teknolojia na ujasiriamali, ikiwemo kutengeneza mtambo wa kutengeneza barabara, sabuni na chaki zinazozalishwa na wanafunzi shuleni hapo.
> “Nimefurahishwa kuona vijana hawa wakitumia elimu kwa vitendo.Nimefurahi kuona kijana akibuni na kutengeneza sabuni,huu ni utekelezaji mkubwa wa takwa la serikali kupitia mtaala mpya.Ubunifu kama huu ndio unaojenga taifa lenye vijana wabunifu na wasio tegemezi,” alisema Kiluvia.
Aidha, aliipongeza shule hiyo kwa mpango wake wa kupanua miradi ya uzalishaji wa sabuni na chaki, akisisitiza kuwa miradi hiyo ikiendelezwa vizuri inaweza kuwa chanzo cha mapato kwa shule na kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujitegemea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Nakido, Haruna Kakiva, alisema mafanikio ya shule hiyo yametokana na ushirikiano wa walimu, wazazi na wanafunzi, hali iliyowezesha shule hiyo kufanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.
Kakiva alifafanua kuwa shule hiyo inatekeleza kikamilifu elimu ya Amali kwa kuwafundisha wanafunzi stadi mbalimbali za maisha kama utengenezaji wa sabuni, chaki, ufugaji wa kuku na mbuzi, pamoja na mradi wa matofali unaoendeshwa na wanafunzi wenyewe.
> “Kupitia elimu ya Amali tunawaandaa wanafunzi wawe wabunifu na wenye uwezo wa kujiajiri. Kwa sasa hatununui chaki, tunazalisha wenyewe, na tunapanga kuanza kuuza bidhaa hizo nje ya shule,” alisema Kakiva.
Mmoja wa wahitimu, Prisca Laizer, alisema elimu waliyoipata imewajenga kiutendaji na kuwapa ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya shule.
> “Tumefundishwa jinsi ya kutengeneza bidhaa kama sabuni na chaki. Tunatoka hapa tukiwa na ujuzi wa kujitegemea, sio kutegemea ajira pekee,” alisema Prisca.
Naye mzazi, Mzee Mollel, aliipongeza shule hiyo kwa malezi bora na ufundishaji wa vitendo unaowaandaa wanafunzi kuwa watu wa kutegemewa katika jamii.
> “Sisi wazazi tunajivunia kuona watoto wetu wanahitimu wakiwa na ujuzi wa vitendo. Hii ni elimu inayojenga kizazi chenye maarifa na ujasiri,” alisema.
Mahafali hayo yalihitimishwa kwa burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa shule hiyo, ikiwemo maonesho ya bidhaa walizotengeneza kupitia miradi ya elimu ya Amali, jambo lililopongezwa na wazazi na wageni waalikwa.
Ends.






















0 Comments