By Arushadigital-SIHA
MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, Daud Ntuyehabi, ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kudaiwa kumchoma kisu tumboni mtu mmoja aitwaye Abdul Issa Mohamed.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa na kuchapishwa kupitia ukurasa rasmi wa jeshi la polisi, tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 7, saa 1:30, katika kijiji cha Kilingi, Kata ya Sanya Juu, wilayani Siha.
Imeelezwa kuwa, mauaji hayo yalitokea baada ya Daud Wilbard Ntuyehabi (marehemu) kumchoma kisu tumboni na kusababisha utumbokutoka nje Abdul Issa Mohamed mkazi wa Kilingi kata ya Sanya juu wilayani humo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliokuwepo kati ya Daudi na mtu mwingine wakidaina fedha wakati wakiwa wanakunywa pombe na Issa Hamad Mohamed alijaribu aliingilia kati kuwatuliza ndipo akachomwa kisu na Daud.
Kufuatia tukio hilo, jeshi la polisi limewakamata watu wanane wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Ntuyehabi. Watuhumiwa hao ni: Hamad Issa Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paul, Shadrack Emanuel, Jeremia Mnkondo, Zainab Elisha, na Issa Mohamed.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini undani wa tukio hilo la kujichukulia sheria mkono.
Ends...

0 Comments