MAMA POLEPOPE AIBUKA MAHAKAMANI LEO "NAOMBA SERIKALI ITUAMBIE ALIPO MWANANGU POLEPOLE"

 Na Arusha Digital – Dar es Salaam


Mama mzazi wa mwanasiasa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, Bi. Anna Mary, amefika leo asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, kushuhudia kuanza kusikilizwa kwa maombi ya dharura kuhusu madai ya kutekwa kwa mwanawe.

Maombi hayo yaliwasilishwa na Wakili Peter Kibatala chini ya hati ya dharura, yakiiomba Mahakama Kuu itoe amri ama Polepole afikishwe mahakamani, au mamlaka husika zieleze alipo na hali yake kwa sasa.


Kwa mujibu wa hati ya maombi yaliyosajiliwa kwa namba 24514 ya mwaka 2025, shauri hilo limepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi.

Katika maelezo yake kwa Mahakama, Wakili Kibatala amedai kuwa Polepole alitekwa nyara alfajiri ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025, kutoka katika makazi yake eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, na watu wanaodaiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi la Tanzania.

Kibatala amesema tukio hilo limeleta hofu kubwa kwa familia na jamii, kwani hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka kwa vyombo vya dola kuhusu alipo mwanasiasa huyo.

“Tunaomba Mahakama iingilie kati mara moja kwa sababu huu ni ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu. Hatuwezi kukaa kimya wakati raia anachukuliwa na watu wanaodaiwa kuwa askari, kisha anapotea bila maelezo yoyote,” alisema Kibatala mbele ya Mahakama.

Wakili huyo amesisitiza kuwa Polepole hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika Mahakama yoyote nchini, hivyo kuendelea kumshikilia pasipo maelezo ni kinyume cha sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Bi. Anna Mary, mama mzazi wa Polepole, alishindwa kujizuia machozi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, akisema familia imeishi kwa hofu tangu siku ya tukio.

“Ni mateso makubwa kwa mama kumtafuta mwanaye asiyefahamika alipo. Naomba Serikali itoe kauli, kama kweli wanamshikilia wamwonyeshe hadharani, lakini kama hajulikani alipo basi watueleze ukweli,” alisema kwa majonzi.

Maombi hayo yamewasilishwa dhidi ya wajibu maombi watano, wakiwemo:

  1. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
  2. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP)
  3. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
  4. Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RCO)
  5. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RPC)

Hadi kufikia muda wa kufungwa kwa taarifa hii, Mahakama ilikuwa haijaanza rasmi kusikiliza maombi hayo, huku ndugu, jamaa na wafuasi wa Polepole wakiwa wamefurika katika viunga vya Mahakama hiyo wakiwa na mabango yaliyosomeka “Haki kwa Polepole ni Haki kwa Wote.”

-Ends..

Post a Comment

0 Comments