GHATI MEMORIAL SCHOOL YAADHIMISHA MAHAFALI YA NNE YA DARASA LA SABA KWA KISHINDO

 Na Joseph Ngilisho- ARUSHA


SHULE ya Ghati Memorial School imefanya mahafali ya nane ya kuvutia ya wahitimu wa Darasa la Saba na Kidato cha Nne, hafla iliyojawa na furaha, shangwe na taswira ya mafanikio makubwa ya wanafunzi waliomaliza ngazi hizo muhimu za elimu.

Mahafali hayo yaliyofanyika leo Oktoba 3,2025 katika viwanja vya shule hiyo, yalihudhuriwa na mamia ya wazazi, walezi na wageni waalikwa, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa shule hiyo, Michael Kimbaki, ambaye alitoa nasaha zenye mguso mkubwa kwa wahitimu wote.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kimbaki aliwataka wahitimu kuzingatia maadili mema, kuheshimu wazazi na walezi waliowalea kwa upendo na kujitolea, pamoja na kuendelea kusimamia nidhamu waliyopata shuleni hapo.

> “Nawasihi muendelee kuwa na nidhamu, mzingatie yale yote mliyofundishwa na msikate tamaa katika safari ya maisha. Maisha ni mapambano, lakini wenye bidii na maadili njema daima hufanikiwa,” alisema Kambeki huku akipigiwa makofi na wazazi na wanafunzi.


Aidha, aliwataka vijana hao kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kupoteza mwelekeo wao kielimu na kimaadili, akisisitiza kuwa elimu ni nguzo muhimu katika kufanikisha ndoto zao za baadaye.

Katika tukio hilo, wanafunzi walionyesha burudani mbalimbali zenye ubunifu wa hali ya juu, ikiwemo nyimbo, ngoma za asili, maigizo na mashairi yaliyoakisi thamani ya elimu na nidhamu. Wazazi na wageni waalikwa walionekana kufurahia kwa shangwe, wakipiga makofi na kusherehekea mafanikio ya watoto wao.

Wahitimu walikabidhiwa vyeti vya kutambua mafanikio yao, huku wakitoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi wa shule, walimu na wazazi waliowasaidia kufika hatua hiyo muhimu.

> “Tunamshukuru Mkurugenzi wetu Bw. Kambeki kwa mazingira mazuri ya kujifunzia, walimu wetu kwa juhudi zao, na wazazi kwa kutuunga mkono. Tunaahidi kuendelea kuwa mabalozi wema wa Ghati Memorial School,” alisema mmoja wa wahitimu kwa niaba ya wenzake.


Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Beata Shirima alitumia nafasi hiyo kumpongeza kila mhitimu kwa kufanikisha safari ya elimu hadi hatua hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea na misingi bora waliyojifunza shuleni hapo.

> “Wahitimu wetu mmeonesha nidhamu, bidii na kujituma kwa kiwango cha juu. Hii ndiyo roho ya Ghati Memorial School. Tunajivunia kuona mmefika hapa leo mkiwa na tabia njema na uelewa mpana. Endeleeni kutembea kifua mbele mkijua elimu yenu ni silaha ya mafanikio,” alisema Mwalimu Mkuu.


Aidha, alitoa shukrani kwa wazazi kwa ushirikiano wao katika malezi na maendeleo ya wanafunzi, huku akiwapongeza walimu wote kwa kujitoa kufundisha kwa moyo wa kujenga taifa lenye maarifa.

Mahafali hayo yalihitimishwa kwa picha za kumbukumbu, zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi, pamoja na maneno ya pongezi kutoka kwa wazazi waliothibitisha kuridhishwa na ubora wa elimu na malezi yanayotolewa na shule hiyo.

Ghati Memorial School imeendelea kujipatia sifa kubwa kutokana na nidhamu, ubora wa taaluma na malezi bora kwa wanafunzi na matokeo bora kwa wanafunzi wanaohitimu, ikiendelea kuwa nguzo imara katika kuandaa kizazi chenye maadili na ujuzi kwa taifa.






-Ends...

Post a Comment

0 Comments