HALI ya simanzi imetanda katika Jeshi la Polisi jijini Arusha baada ya Askari wa Kituo Kikuu cha Polisi, Omary Mnandi, kuuawa kikatili kwa kupigwa na kitu kizito kichwani katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia leo maeneo ya Bar maarufu ya Picnic, eneo la Kaloleni, jijini Arusha.
Marehemu MNANDIKwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka chanzo chetu ndani ya jeshi hilo, marehemu Mnandi alikuwa akiwa na wenzake wakijiburudisha kwa vinywaji vya pombe katika bar hiyo kabla ya mauti kumkuta.
Inaelezwa kuwa majira ya saa sita usiku, marehemu alizidiwa na kilevi na kuamua kwenda kupumzika ndani ya gari lake. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, alifungua na kuingia katika gari jingine lililokuwa jirani bila kujua kuwa si lake.
Mashuhuda wanasema kuwa alipolala usingizi mzito ndani ya gari hilo, wamiliki wa gari waliporejea muda mfupi baadaye walishangazwa kumkuta mtu asiyejulikana akiwa amelala ndani. Katika hali ya taharuki, walimshambulia kwa kipande cha chuma wakidhani ni jambazi, na kumsababishia majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake papo hapo.
Baada ya tukio hilo, askari wenzake waliokuwa naye walipokea taarifa za mauaji hayo na kufika eneo la tukio ambapo waliwakamata washukiwa watatu wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru (Moshwale), huku watuhumiwa wakishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa marehemu Mnandi alikuwa akiishi katika nyumba za askari polisi (line polisi) eneo la Fire, jijini Arusha, na anatarajiwa kusafirishwa kwa mazishi mkoani Tanga, alikozaliwa.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justin Masejo, ili kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu tukio hilo zinaendelea.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Richard, ambaye alikuwa miongoni mwa wateja waliokuwapo katika eneo hilo, alisema tukio hilo lilitokea kwa mshituko mkubwa na wengi hawakujua kilichokuwa kinaendelea.
> “Tulidhani kuna jambazi ameiba gari, watu wakaanza kukimbia huku wengine wakipiga kelele. Baadaye tulisikia mtu amepigwa vibaya, kumbe ni askari wetu. Ni tukio la kusikitisha sana,” alisema Richard kwa uchungu.
> “Inaumiza zaidi kuona maisha ya mtu yanapotea kwa makosa madogo kama haya. Tunaiomba serikali iongeze elimu ya utulivu na mawasiliano katika maeneo ya starehe,” aliongeza.
Tukio hilo limezua majonzi makubwa miongoni mwa askari na wakazi wa jiji la Arusha, wengi wakieleza kusikitishwa na namna maisha ya askari huyo yalivyokatishwa kwa ukatili mkubwa.
POLISI YATHIBITISHA KUSHIKILIA WATANO
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limethibitisha kuwashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za mauaji ya Omary Mnandi (30) Askari Polisi Mkazi wa Jiji la Arusha.
Akitoa taarifa hiyo leo Oktoba 12, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 12, 2025 muda wa usiku huko katika Bar iitwayo Simaloi iliyopo maeneo ya Kaloleni Jijini Arusha.
SACP Masejo amebainisha kuwa watuhumiwa hao walimjeruhi mhanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kupelekea umauti wake wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha.
Aidha, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni baada ya Omary Mnandi (marehemu) kutokana na unywaji wa pombe ambao ulipelekea kukosea uhakika wa gari lake Na. T. 402 CNC na kuingia kwenye gari Na. T. 734 AXR la mmoja wa watuhumiwa hao na ndipo walianza kumshambulia.
Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linakamilisha uchunguzi wa tukio hilo ili hatua nyingine za kisheria zifuatwe.
Mwisho.



0 Comments