WATU TISA WAFARIKI DUNIA KWA AJALI MBAYA CHEMBA,WAMO WANAFUNZI WANNE!

Watu Tisa Wafariki Ajali Mbaya Chemba, Wanafunzi Wanne Wamo

By Arushadigital -DODOMA


Dodoma – Watu tisa wamepoteza maisha, wakiwemo wanafunzi wanne, huku wengine 16 wakijeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Kambi ya Nyasa, wilayani Chemba mkoani Dodoma.


Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria aina ya Tata, mali ya Kampuni ya Babuu Trans lenye namba za usajili T129 DVX, na lori la mizigo aina ya Fuso namba T907 EJZ.


Kwa mujibu wa mashuhuda, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye aliharakisha kupita bila tahadhari na hatimaye kupoteza mwelekeo, kisha kuingia upande wa basi lililokuwa limebeba abiria.


Kauli ya Mkuu wa Mkoa


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alithibitisha vifo hivyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.


“Ajali hii ilisababisha vifo vya watu watano papohapo na majeruhi 20. Wakati wakiendelea kupatiwa huduma, wanne kati ya majeruhi hao walifariki dunia wakiwa njiani kuhamishiwa Hospitali ya Rufani, na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia watu tisa, huku majeruhi wakibaki 16,” alisema Senyamule.


Ameeleza kuwa kati ya majeruhi 16, tisa walipelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na hali zao zinaendelea vizuri, huku wengine wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba.


Pole na Shukrani


Senyamule ametoa pole kwa familia za marehemu na wote walioathirika, akiwashukuru wananchi, viongozi wa wilaya, Jeshi la Polisi na wataalamu wa afya kwa msaada mkubwa walioutoa katika uokoaji na kuwahudumia majeruhi.

Ends ..

Post a Comment

0 Comments