MAKONDA AANZA KUTEMA CHECHE AMVAA MKURUGENZI WA JIJI ARUSHA, AMPA WIKI MOJA KULIPA MADENI ANAYODAIWA,MGOMBEA UDIWANI MURIET AWASHA MOTO

Makonda Amvaa Mkurugenzi wa Jiji: Atoa Wiki Moja Kulipa Malimbikizo ya Wenyeviti wa Mitaa

Na Joseph Ngilisho, Arusha

Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paulo Makonda, ameonekana kana kwamba ameanza kutekeleza majukumu yake ya kibunge hata kabla ya kuapishwa, baada ya kutoa agizo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, kuhakikisha analipa malimbikizo ya miezi sita wanayodaiwa na wenyeviti wa mitaa.



Makonda alitoa kauli hiyo leo, Alhamisi Septemba 18, 2025, katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni uliofanyika katika eneo la Soko la Kwa Morombo, Kata ya Muriet, jijini Arusha.


Awali, madai hayo yaliibuliwa na mgombea udiwani wa kata hiyo, Kredo Kifukwe, aliyesema malimbikizo hayo yamekuwa mzigo mkubwa kwa wenyeviti wa mitaa na kuathiri ufanisi wao katika kuwahudumia wananchi.


“Mkinichagua, ndani ya wiki moja nitahakikisha nashughulikia malipo ya wenyeviti wa mitaa ambao hawajalipwa kwa zaidi ya miezi sita,” alisema Kifukwe katika salamu zake.


Kauli hiyo ilimfanya Makonda kusitisha mpango wake wa kuwatambulisha wagombea udiwani wengine 25 aliokuwa amewapandisha jukwaani na badala yake kutoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Jiji.


“Jamani, mnaniruhusu nianze majukumu yangu kabla sijaapishwa?” alihoji Makonda huku wananchi wakijibu kwa sauti ya juu, “Ndiooo!”


Akisisitiza msimamo wake Makonda alisema,“Kuanzia leo, natoa wiki moja kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kuhakikisha anawalipa watendaji wote wa mitaa malimbikizo yao. Wanadai fedha zao, na lazima walipwe.”


Kauli hiyo ilishangiliwa kwa nguvu na wananchi waliohudhuria mkutano huo, wakimpongeza Makonda kwa kuonyesha uthubutu wa kutetea maslahi ya viongozi wa ngazi ya mitaa hata kabla ya kuingia rasmi bungeni.

Mmoja wa wananchi waliokuwepo, Bi. Hawa Mollel mkazi wa Muriet, alisema:

“Tunachohitaji ni viongozi wenye msimamo na ujasiri wa kutusemea. Kauli ya Makonda imetupa matumaini kuwa akipewa ridhaa ataweka maslahi ya wananchi mbele kuliko maneno matupu.”







Ends..

Post a Comment

0 Comments