Na Joseph Ngilisho, Karatu
WANAFUNZI wa Shule ya Ms ingi ya Tumaini Junior wilayani Karatu, mkoani Arusha, wameibua matumaini mapya katika sekta ya huduma za maji baada ya kubuni mfumo wa kipekee wa ulipaji maji kwa kutumia simu ya mkononi kabla ya matumizi.
Ubunifu huo uliofanywa na wanafunzi hao shuleni hapo wakishirikiana na wenzao wa Tumaini Senior sekondari, unalenga kumrahisishia mteja huduma ya ulipaji bili za maji kwa haraka, uwazi na usalama zaidi, tofauti na mfumo wa sasa unaotumia muda mrefu na mara nyingi hukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiankara.
Akiongea wakati wa maonesho ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika shuleni hapo na kwenda sanjari na Mahafali ya 15 ya kumaliza elimu ya msingi, kinara wa mradi huo, Lepapa Alaisi, alisema somo la ziada la sayansi na ubunifu pamoja na fursa ya kusomea somo la sayansi ya kompyuta tangu kidato cha kwanza, ndizo zilizopelekea wao kubuni mfumo huo.
> “Tuliona changamoto inayowakabili wateja wa maji, hasa muda mrefu unaotumika kwenye ulipaji wa ankara. Tukajiuliza kwa nini tusitengeneze mfumo rahisi wa kidijitali ambao mtu atakuwa analipia kabla ya kutumia maji kupitia simu yake ya mkononi. Ndipo wazo hili likaibuka,” alisema Alaisi.
> “Ni fahari kuona watoto wadogo wakibuni suluhisho linaloweza kubadili maisha ya jamii. Ni jukumu letu wazazi na viongozi kuhakikisha tunawaendeleza vijana hawa na vipaji vyao visipotee bure,” alisema Akyoo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule za Tumaini senior na Tumaini Junior, Modest Bayo, alisema shule yake imekuwa ikitoa kipaumbele kikubwa katika masomo ya sayansi na teknolojia, hatua ambayo imewasaidia wanafunzi kuwa wabunifu na hata kupata ajira mapema.
> “Watoto wetu wa Tumaini Senior wakianza kidato cha kwanza wanaanza na somo la sayansi ya kompyuta. Somo hili sasa limeingizwa rasmi katika mtaala mpya wa elimu nchini, jambo ambalo limewasaidia wahitimu wetu kupata ajira hata baada ya kumaliza kidato cha nne. Tayari tuna wahitimu wanne waliopata nafasi ya kufanya kazi na kampuni ya Google kutokana na umahiri wao katika teknolojia,” alisema Bayo.
Wataalamu wa sekta ya maji na teknolojia wanasema iwapo mfumo huu utaboreshwa na kupewa nafasi ya kutumika kitaifa, unaweza kuleta mageuzi makubwa kwa wananchi na mamlaka husika.
Utapunguza adha ya foleni ndefu na safari za mara kwa mara kwenda ofisini kulipia bili za maji.
Mteja ataweza kulipia maji akiwa nyumbani au popote kupitia simu ya mkononi, jambo litakaloongeza urahisi na uhakika wa kupata huduma.
Mfumo huu pia unatoa uwazi wa matumizi, kwani kila mteja atalipa kabla ya kutumia maji, hivyo kupunguza migogoro ya ankara na madai ya bili zisizoeleweka.
Utasaidia kuongeza mapato ya mamlaka kwa sababu malipo yanahakikishwa kabla ya huduma kutolewa, hivyo kupunguza madeni sugu ya wateja.
Unarahisisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kidigitali, jambo litakalopunguza gharama za uendeshaji.
Ubunifu huu wa wanafunzi wa Tumaini Senior umechukuliwa kama kielelezo cha namna elimu ya sayansi na teknolojia inavyoweza kuleta mageuzi makubwa katika jamii endapo itatiliwa mkazo.
Wadadisi wa elimu wanasema tukio hili ni ishara kuwa mageuzi ya kidigitali Tanzania yanapaswa kuanzia shuleni, kwa kuwapa vijana fursa ya kujifunza kwa vitendo na kutumia elimu yao kutatua matatizo ya jamii.
Ends...
0 Comments