CCM ARUSHA YAPITISHA MADIWANI 160 KWA UCHAGUZI MKUU OKTOBA
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kimepitisha jumla ya madiwani 160 watakaowania nafasi za udiwani katika kata mbalimbali za majimbo saba ya mkoa huo kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Ramsey Saipurani, alisema wagombea waliopitishwa walipatikana baada ya mchujo uliozingatia vigezo vya uadilifu, uchapakazi, uzoefu, historia ndani ya chama na kukubalika kwa wananchi.
> “Wagombea walioteuliwa ni wale walioonyesha kujituma, kuthamini maadili ya chama na kuungwa mkono na wananchi katika maeneo yao. Tunawaomba wanachama wote kuwaunga mkono wagombea hawa,” alisema Saipurani.
Alisisitiza kuwa muda wa malumbano umekwisha na sasa ni wakati wa mshikamano ili chama kipate ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, katika Jimbo la Arusha Mjini, Kata ya Olasiti, bado hakujapatikana mgombea rasmi kutokana na sintofahamu miongoni mwa wagombea, ambapo suala hilo limepelekwa kwa ngazi za juu za chama kwa uamuzi zaidi.
Aidha, malalamiko yaliyotolewa kuhusu uteuzi wa madiwani wa viti maalumu katika Tarafa ya Elerai pia yamewasilishwa kwa vikao vya juu vya chama ili kufanyiwa uamuzi wa mwisho.
Taarifa zinaonesha kuwa katika Jimbo la Arusha Mjini, madiwani 14 waliokuwa wakihudumu awali hawakupitishwa. Nafasi zao zimechukuliwa na wagombea wapya katika kata za Moshono, Olmot, Sombetini, Sekei, Ngarenaro, Themi, Engutoto, Terat, Muriet, Sokoni One, Sinoni, Sakina, Levolosi na Lemara.
Kwa upande wa Jimbo la Longido, Katibu Mwenezi wa wilaya hiyo, Solomoni Lekui, alisema madiwani sita wa zamani pia hawakupitishwa baada ya kushindwa kupata nafasi za juu kwenye kura za maoni au kukosa sifa za kimaadili.
Kata hizo ni pamoja na Kamwanga, Engikaret, Namanga, Engarenaiobo, Ketumbeine na Iloirienito.
CCM Mkoa wa Arusha imesisitiza kuwa uteuzi huo unalenga kuleta nguvu mpya na kuimarisha chama kuelekea Uchaguzi Mkuu. Wanachama na wapenzi wa chama wameombwa kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha ushindi katika majimbo yote.
Ends...
0 Comments