WAMERU HUWAAMBI KITU KWA NASARY WATOA TAMKO ZITO LA KUMUUNGA MKONO UBUNGE , RAIS SAMIA NAYE KUOMBEWA KURA ,VIONGOZI WA DI WAMWAGA MAOMBI NASARI ATOKWA MACHOZI DC ASHUHUDIA!

WAMERU WAKUSANYIKA MRINGARINGA KUMUUNGA MKONO NASARI

Na Joseph Ngilisho-ARUMERU

JAMII ya Wameru ikiongozwa na viongozi wa mila (Washili), viongozi wa dini, serikali na chama cha Mapinduzi (CCM), wamekusanyika katika mti wa mila wa Mringaringa uliopo Kata ya Poli, Jimbo la Arumeru Mashariki na kwa kauli moja kukubaliana kumuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo Joshua Nasari, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na madiwani wa chama hicho.

Mkutano huo mkubwa  umefanyika leo Septemba 8,2025 na kuvutia zaidi ya wananchi 300,000 ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi, viongozi wa dini na marika mbalimbali ya jamii, ukiashiria mshikamano wa kipekee kwa Wameru.

Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu la kikao kilichoongozwa na viongozi wa mila lilikuwa ni kuimarisha mshikamano, kuondoa makundi ya kisiasa yanayogawa jamii na kuelekeza nguvu katika maendeleo ya pamoja.

Mshiri Mkuu wa Wameru, Willson Mbise, alitangaza rasmi kuungwa mkono kwa Nasari kwa asilimia mia moja.

> “Mgombea wetu ambaye amepitishwa na Chama Cha Mapinduzi tunatakiwa tumuunge mkono kwa dhati. Wote tuliofika hapa zaidi ya 300,000 tuwe mbegu ya kushawishi wengine waliopo majumbani ili kumhakikishia ushindi,” alisema Mshiri Mkuu.

Katika tukio hilo lililoamsha hisia, Askofu wa Kanisa la AMEC, Yuda Pallangyo, aliongoza maombi ya  kumuombea Joshua Nasari pamoja na familia yake. Maombi hayo yalimgusa mgombea huyo kiasi cha kutokwa machozi akiwa ameshika mkono wa mkewe mbele ya umati.

> “Tunatamani kuona Meru yenye mshikamano na maendeleo. Joshua, nenda ukapiganie jamii hii bungeni kwa masilahi ya kila mmoja wetu,” alisema Askofu Pallangyo, akipokelewa kwa shangwe kubwa.


Baada ya maombi hayo, wazee wa mila na viongozi wa dini walimzawadia Nasari zawadi maalumu kama ishara ya shukrani na heshima kwa uamuzi wake wa kugombea ubunge wa Arumeru.


Kwa upande wake, Nasari alisema ameamua kuacha nafasi ya ukuu wa wilaya ili kuwatumikia moja kwa moja Wameru.

> “Nikiwa Mbunge nitashirikiana na Mkuu wetu wa Wilaya kuhakikisha tunaleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo. Meru tumechelewa, sasa ni wakati wa kupiga hatua. Changamoto za maji na barabara lazima zitatuliwe,” alisema Nasari kwa sauti ya kipekee iliyojaa hisia.


Aidha, Nasari aliahidi kuunda Baraza la Ushauri la Meru litakaloshirikiana naye katika kufanikisha mipango ya maendeleo jimboni humo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mwinyi Ahmed Mwinyi aliwahimiza wananchi wa jamii hiyo kushikamana na kulinda mshikamano wao.

> “Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yanatakiwa yailetee Meru ustawi zaidi. Tukishirikiana tutalinda mila zenye tija na kuhakikisha jamii yetu inapiga hatua,” alisema Mwinyi.

            









Ends...

Post a Comment

0 Comments