WAKURUGENZI WAAGIZWA KUWAWEZESHA WAMACHINGA KUPATA ELIMU YA MIKOPO

Na Joseph Ngilisho, Arusha

WAKURUGENZI watendaji wa halmashauri zote saba za Mkoa wa Arusha wametakiwa kuwawezesha wataalamu wa Sekta za Maendeleo ya Jamii, Biashara na TEHAMA ili kuwafikia wafanyabiashara wadogo na wamachinga kwa kuwapa elimu ya mikopo isiyo na riba na kuepuka kuingia katika mikopo ya ukatili.

Rai hiyo imetolewa leo September 3,2025 na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha (RAS), Misaile Albano Mussa, wakati akifungua Tamasha la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga) mkoani humo, lenye lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara hao na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulitambua kundi hilo na kuliwezesha kupitia mikopo yenye masharti nafuu.

Mussa alisema kuwa iwapo wataalamu hao watawezeshwa ipasavyo na kuwekwa katika mikakati ya kutoa elimu kwa wamachinga, itasaidia kuwatambua, kuwaunganisha na kuwafungulia fursa mbalimbali za kiuchumi. Aidha, itawajengea sifa stahiki za kupata mikopo nafuu badala ya kuendelea kuteseka na mikopo yenye riba kubwa inayowavunja moyo na kuwapotezea malengo ya kujikwamua kiuchumi.

> “Nitoe wito kwa wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha wanalifikia lengo la Serikali la kuwawezesha wamachinga kupata elimu ya mikopo na uendeshaji wa biashara zao. Hii itasaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema.



Aidha, alibainisha kuwa hadi sasa ni wafanyabiashara 224 pekee waliokwisha chukua mikopo hiyo, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na fedha zilizotengwa, hivyo kuna haja ya kuongeza nguvu ya kuwafikia wengi zaidi.

Kwa upande wao, wamachinga walimpongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa alizozifanya katika kulitambua kundi hilo na kuliunganisha na fursa za kibiashara. Walisema hatua ya Serikali kuwapatia mikopo nafuu ni mkombozi mkubwa kwao.

Serikali ya Rais Samia imetenga shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya wamachinga nchini kote, ambapo mkoani Arusha pekee wamachinga na wafanyabiashara wadogo wamepatiwa zaidi ya shilingi milioni 501.

Ends...

Post a Comment

0 Comments