WAHIFADHI MNA DHAMANA YA KULINDA RASILIMALI ZA TAIFA – RC MAKALLA
Na Joseph Ngilisho-KARATU
MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amewataka watumishi na viongozi wa mamlaka za hifadhi za taifa mkoani humo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na uzalendo, akisisitiza kuwa wanabeba dhamana kubwa ya kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha uendelevu wa vivutio vya utalii.
Akizungumza leo Jumamosi, Septemba 20, 2025, katika makao makuu ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, wilayani Karatu, wakati alipokutana na menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), RC Makalla alisema jukumu la uhifadhi ni msingi wa maendeleo ya sekta ya utalii ambayo Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipa msukumo mkubwa.
> “Nyie ni mabalozi wazuri wa taifa. Hakikisheni mnalinda hifadhi zetu kwa uadilifu na uzalendo. Utalii ni matokeo ya uhifadhi, hivyo ni lazima tuendelee kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais ambazo zimewezesha ongezeko kubwa la idadi ya watalii kwenye hifadhi zetu,” alisema RC Makalla.
Mbali na kusisitiza usimamizi wa sheria na mipaka ya hifadhi kwa uadilifu, Makalla pia aliahidi ushirikiano wa karibu na wahifadhi hao. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu endelevu kwa jamii kuhusu uhifadhi na kuimarisha mahusiano bora na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi.
Kwa upande wao, Yustina Kiwango, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, na Witness Shoo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, walibainisha kuwa idadi ya watalii imeongezeka maradufu katika hifadhi hizo, hali ambayo imechangia kuongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa mkoa.
Walieleza kuwa mafanikio hayo yametokana kwa kiasi kikubwa na filamu maarufu za The Royal Tour na Amazing Tanzania zilizochezwa na Rais Dkt. Samia, ambazo zimeitangaza vyema Tanzania kimataifa na kuongeza hamasa ya watalii kutembelea vivutio vya asili.
Ends.....
0 Comments