Kredo Kifukwe Azindua Kampeni za Udiwani Muriet kwa Kishindo
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Muriet kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kredo Kifukwe, ameanza kampeni zake kwa kishindo, akiahidi kusimamia kikamilifu maendeleo ya kata hiyo na kuonya wakandarasi wazembe pamoja na taasisi zinazoshindwa kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Katika uzinduzi huo uliofanyika Muriet lep jumamosi septemba 20,2025, Kifukwe alikabidhiwa rungu la kimila kama ishara ya kuaminiwa na wananchi kuwa kiongozi wao. Akihutubia mamia ya wananchi wa kata hiyo, alisema rungu hilo litakuwa alama ya kusimamia uwajibikaji na kuwashughulikia watendaji wazembe wanaoshindwa kuwatumikia wananchi.
> “Barabara zetu ni mbovu sana. Nikiingia madarakani, wakandarasi wababaishaji wajipange, maji ya ugali hayaonjwi. Nitahakikisha kila aliyepewa dhamana ya kusimamia maendeleo anawajibika kweli kweli. Tutahakikisha Muriet inashtua kwa maendeleo,” alisema Kifukwe kwa msisitizo.
Aidha, alikosoa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (Auwsa) kwa kushindwa kutoa huduma ya uhakika ya maji safi na salama kwa wananchi wa kata hiyo.
Kifukwe alisema iwapo ataingia katika Baraza la Madiwani hatakuwa na mzaha, akionya watendaji wanaopenda kujifungia ofisini na kusahau shida za wananchi kwamba “atawachangamsha kwa kuwaamsha usingizini.”
Akizungumza kuhusu maendeleo ya taifa, Kifukwe alimsifu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa zilizotekelezwa chini ya uongozi wake, akibainisha kuwa mafanikio hayo yamewarahisishia wagombea wa CCM kuomba kura kwa wananchi.
Pia alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paulo Makonda, akisema ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kiutendaji na ubunifu.
> “Tumepewa Makonda Arusha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Ni kiongozi mwenye akili nyingi na ubunifu wa hali ya juu. Kufanya kazi na mbunge wa aina hiyo ni bahati kubwa, tunamwona kama lulu ya Arusha. Maendeleo lazima yajulikane,” alisema Kifukwe huku akishangiliwa na wafuasi wake.
Mbise: Sina Kinyongo, Nampigia Kredo Debe
Aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Francis Mbise, alimhakikishia Kifukwe ushirikiano, akimpongeza kwa kuteuliwa kuwania nafasi hiyo na kukanusha madai kuwa ana kinyongo.
> “Wanaosema nina kinyongo na Kredo wasitupotezee muda. Nimekonda kweli? Haya ni maneno ya wapambe. Nipo imara na moyo wangu ni mweupe. Nipo tayari kumpigia debe nyumba kwa nyumba ili ashinde kwa kishindo,” alisema Mbise kwa utani uliowachekesha wananchi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Chiku Issa, aliwataka wananchi wa Muriet kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Kifukwe, akisema ndiye chaguo sahihi litakalohakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana.
> “Kredo ni kiongozi jasiri na mwenye maono makubwa. Anayo dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake. Tukimpa ridhaa ataibadilisha Muriet na kuifanya kuwa mfano wa maendeleo Arusha. Naomba tushirikiane kumpa kura za kishindo,” alisema Mbunge huyo.
Mmoja wa wananchi wa Muriet, Zaituni John, akizungumza baada ya mkutano huo alisema wanatarajia kuona mabadiliko makubwa endapo Kifukwe atachaguliwa kuwa diwani.
> “Tuna imani naye kwa sababu ameonyesha nia ya dhati ya kushughulikia kero zinazotusumbua kila siku, hasa barabara na maji. Tunataka kiongozi ambaye atakuwa karibu na wananchi, siyo wa kujifungia ofisini. Sisi kama wananchi tuko tayari kumpa kura zetu,” alisema Zaituni huku akipigiwa makofi na wenzake.
Ilani ya CCM
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM, Saipulani Ramsey, alimkabidhi rasmi Kifukwe ilani ya chama, akimtaka kuhakikisha anasimamia utekelezaji wake endapo atachaguliwa.
Ramsey alisisitiza kuwa mgombea huyo anatakiwa kupigania upatikanaji wa huduma za maji safi, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, elimu, afya na mikopo ya kijamii ili wananchi wa Muriet wanufaike moja kwa moja na uongozi wake.
> “Kila kitu kipo ndani ya ilani ya CCM. Kifukwe akishinda akihakikishe wananchi wananufaika na ilani hii, ndipo faida ya kukichagua chama cha Mapinduzi itakapoonekana,” alisema Ramsey.
Ends...
0 Comments