Vuta Nikuvute Mahakamani: Wanachama wa CHADEMA Wazuiliwa Kuingia
By Arushadigital-Dar es salaam.
Katika kile kinachoonekana kama mvutano kati ya wananchi na vyombo vya dola, baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamezuiliwa kuingia ndani ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambako kesi ya Mwenyekiti wao inaendelea kusikilizwa.
Sababu iliyotolewa na mamlaka ni kwamba ukumbi wa mahakama ni mdogo, hivyo hauwezi kuchukua watu wote waliotaka kushuhudia mwenendo wa shauri hilo. Hata hivyo, wanachama hao wamelalamika kuwa nafasi nyingi ndani ya ukumbi huo zimejazwa na askari polisi badala ya wananchi.
“Tunalalamika kwa sababu tuna haki ya kikatiba kushiriki na kusikiliza kesi ya kiongozi wetu, lakini tunazuiwa kwa kisingizio cha ukumbi kuwa mdogo, huku askari wakiwa wamejaa ndani,” alisema mmoja wa wanachama aliyeachwa akisubiri nje ya viunga vya mahakama, huku akionekana mwenye masikitiko.
Kwa upande wao, wanachama waliokosa nafasi wameeleza kuwa kitendo hicho kinawanyima haki ya msingi ya kushuhudia kesi ya wazi. Wameitaka Mahakama pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa haki ya wananchi ya kushiriki kwenye mashauri ya wazi inalindwa ipasavyo, hususan pale inapohusu kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa katika jamii.
Kwa sasa, macho na masikio ya wafuasi na wananchi wengi yameelekezwa mahakamani, wakisubiri kuona mwenendo na hatma ya kesi hii ambayo imekuwa gumzo kubwa la kisiasa nchini.
Ends...
0 Comments