TWARIQA YAZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA KUPIGA KURA NCHI NZIMA, KUMPIGIA DEBE RAIS SAMIA, ZIARA YA NAIBU KATIBU MKUU YATUA KWA KISHINDO OLORESHO

TWARIQA YAZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA KUPIGA KURA KUMPIGIA DEBE RAIS SAMIA

Na Joseph Ngilisho, Arusha


TAASISI ya dini ya Kiislamu ya Twariqa imeanza kampeni ya nchi nzima kuhamasisha waumini na wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, ikilenga kumpa ushindi wa kishindo mgombea urais wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Kampeni hiyo inaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Twariqa, Sheikh Haruna Hussein, ambapo akizungumza katika ziara yake ya kwanza kwenye Msikiti wa Oloresho, Kata ya Olmoti jijini Arusha, aliwataka waumini na wananchi kujitokeza kupiga kura kwa kumchagua Rais Samia.


“Sheikh Hussein alisema, ‘Rais Samia ameonesha nia ya dhati ya kuilinda amani ya nchi yetu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kura na kumuunga mkono ili aendelee kuijenga Tanzania yenye mshikamano.’”


Hafla hiyo ilipambwa na futari ya kukata na shoka vyakula mbalimbali, vinywaji na kuchinjwa ng’ombe watatu pamoja na mbuzi kadhaa na ilienda sanjari na dua Maalumu ya kumwombea Rais Samia ili ashinde kwa kishindo uchaguzi mkuu ujao. 


Katika hotuba yake, Sheikh Haruna alisisitiza kuwa viongozi wa dini hawapaswi kushiriki siasa kwa ushabiki wa vyama, bali wasimame kama nguzo ya taifa kwa kukemea upotoshaji unaoenezwa kupitia mitandao ya kijamii.


“Mitandao inatumika vibaya kutukana viongozi wa nchi, hali hii haiwezekani. Viongozi wa dini lazima wasimame kidete kukemea vitendo hivi na kulinda mshikamano wa taifa letu,” alisisitiza huku akishangiliwa na waumini.

Kwa upande wake, Sheikh wa Msikiti wa Oloresho, Juma Maulid, alisema ziara hiyo ni ya baraka kwa jamii na inazidi kuimarisha mshikamano wa waumini. “Tunamshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya, na sisi kama viongozi wa dini tutahamasisha mshiriki wa uchaguzi kwa amani na mshikamano,” alisema.

Naye Balozi wa Mtaa huo , Stewart Temba, aliwapongeza viongozi wa Twariqa kwa kuja kijijini hapo na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia wananchi kutambua wajibu wao wa kidemokrasia. “Ujumbe huu umewafikia wananchi kwa uwazi, kila mmoja ameona umuhimu wa kushiriki kupiga kura ili kumchagua kiongozi anayethamini maendeleo,” alisema Temba.


Baadhi ya waumini waliohudhuria waliungana na kauli hizo, akiwemo Hassan Athumani, mkazi wa Oloresho, aliyesema, “Rais Samia amejitahidi sana kuimarisha miundombinu na huduma za jamii. Ni wajibu wetu kumwombea dua rais Samia  pamoja na nchi yetu ,kumrudisha madarakani ili aendelee na kazi nzuri aliyoianza.”


Vilevile, mama muumini Zainabu Ramadhan, alisisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo. “Sisi akina mama tumeshuhudia maendeleo makubwa kwenye afya na elimu chini ya Rais Samia. Tunapaswa kujitokeza kupiga kura ili kuhakikisha tunaendeleza amani na maendeleo kwa vizazi vyetu,” alisema huku akipigiwa makofi.


Ziara hiyo imebeba ujumbe wa mshikamano, mshikikamo wa kitaifa na heshima kwa viongozi, huku Twariqa ikijipambanua wazi kumuunga mkono Rais Samia kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.









Ends...

Post a Comment

0 Comments