VIDEO YA ASKARI POLISI IKIWAONESHA WAKITESWA YAZUA TAHARUKI , POLISI YATOA TAMKO

Video ya Askari Polisi Akiwa Chini Yazua Taharuki, Jeshi Laahidi Uchunguzi

By Arushadigital 


Video inayoonyesha Askari Polisi akiwa amelala chini imezua taharuki kubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku ikidaiwa kuwa imerekodiwa katika Kituo cha Polisi Bandari.


Katika ujumbe ulioambatana na video hiyo, baadhi ya askari wanaodaiwa kuwa wa kituo hicho walieleza madai ya kunyanyaswa na viongozi wao, wakimtaja Mkuu wa Kituo (OCS) kuwa chanzo cha vitendo vya rushwa na mateso.


Wamedai kwamba askari kadhaa wamekuwa wakifungwa mahabusu bila kosa lolote, kwa sababu tu hawakutoa rushwa, hali ambayo wanasema imekuwa ikiwatia msongo wa mawazo, kukata tamaa na hata kufikiria kuacha kazi au kujitoa uhai.


Jeshi la Polisi latolea ufafanuzi


Kufuatia kusambaa kwa video hiyo, Jeshi la Polisi Tanzania kupitia taarifa yake rasmi ya Septemba 24, 2025, limesema limeiona video hiyo na tayari limeanzisha uchunguzi wa kina kubaini ukweli wake, wapi ilirekodiwa na ni akina nani waliohusika kuiandaa.


Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa mara uchunguzi utakapokamilika, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.


Wananchi waombwa kuwa wavumilivu


Aidha, Jeshi hilo limewataka wananchi kuwa wavumilivu na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, likiahidi kutoa taarifa rasmi mara uchunguzi utakapokamilika.


Ends..

Post a Comment

0 Comments