MATEMBEZI YA SHULE YA GREEN VALLEY YA TIKISA NI SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA 25 , IKIANGAZIA UJUMBE WA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Green Valley yasherehekea Miaka 25 kwa ujumbe wa Amani kuelekea Uchaguzi

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


LEO Septemba 24, 2025 – Shule ya Msingi Green Valley imeadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake kwa njia ya kipekee, baada ya wanafunzi wake kufanya matembezi ya amani jijini Arusha wakiwa na ujumbe mahsusi wa kusisitiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika shamrashamra hizo zilizofanyika leo Jumatano, wanafunzi na walimu wa shule hiyo waliwasili viungani mwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambapo walipokelewa na Mkuu wa Mkoa, CPA Amos Gabriel Makalla.

Akizungumza na wanafunzi hao, RC Makalla aliwapongeza kwa kuadhimisha miaka 25 ya shule yao kwa mtindo wa kipekee unaohamasisha mshikamano na utulivu wa taifa huku akisifu ubunifu uliofanywa na mmiliki wa shule hiyo YAHAYA NJALITA katika kuimarisha Mshikamano .




> “Nataka niwahakikishie kuwa mtasoma kwa amani, mtaishi kwa amani na uchaguzi utafanyika kwa amani. Nawapongeza kwa maadhimisho yenu ya miaka 25 kwa kuhamasisha amani – mkasome kwa utulivu na nchi yetu itaendelea kuwa na amani,” alisema RC Makalla.


Wanafunzi: Amani ndiyo msingi wa elimu

Awali, wanafunzi hao walieleza kuwa walichagua ujumbe wa amani kwa maadhimisho yao kwa sababu bila utulivu, elimu na maendeleo haviwezi kustawi.

> “Amani ndiyo msingi wa elimu na maisha bora. Bila amani, hatuwezi kusoma vizuri, wala kufanikisha ndoto zetu. Tunataka Tanzania iendelee kuwa nchi salama kwa vizazi vyote,” alisema mmoja wa wanafunzi kwa niaba ya wenzake.


Green Valley yapokea pongezi

RC Makalla aliwataka wazazi, walezi na walimu kuendelea kushirikiana katika malezi ya watoto, akisisitiza kuwa jukumu la kudumisha amani ni la kila mmoja.

Shule ya Green Valley, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, imekuwa mstari wa mbele katika kukuza taaluma na malezi bora ya wanafunzi mkoani Arusha, na sasa imetimiza robo karne ikiwa bado inaendeleza ndoto za mamia ya watoto.

> “Maadhimisho ya miaka 25 ya Green Valley yatahitinishwa kesho September 25 katika shule hiyo na yamekuwa kielelezo cha namna taasisi za elimu zinavyoweza kushiriki katika kulinda amani ya taifa,” alihitimisha RC Makalla.







-Ends 

Post a Comment

0 Comments