SAMIA KUPOKELEWA KIJANJA ARUSHA,MAPOKEZI YAKE KUPAMBWA NA HELIKOPTA ATAMWAGIWA MAUA YA HESHIMA ANGANI

Na Joseph Ngilisho – Arusha


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paulo Makonda, amesema maandalizi ya kumpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, yamepangwa kwa upekee usio na kifani, ambapo helikopta maalum itapita angani ikimwaga maua kama ishara ya heshima na mapenzi makubwa ya wananchi kwa Kiongozi wa Taifa.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofurika wananchi leo, Makonda alisema ujio wa Rais Samia jijini Arusha si tukio la kawaida, bali ni sherehe ya kihistoria itakayobaki kwenye kumbukumbu za wananchi wa mkoa huo kwa vizazi vijavyo.

> “Mama yetu Samia atapokelewa tofauti kabisa. Helikopta itapita juu na kumwaga maua juu ya jiji lote la Arusha. Ni namna ya kipekee ya kuonyesha mapenzi yetu kwake. Hakuna atakayebaki bila kujua kuwa Rais yupo Arusha,” alisema Makonda huku akishangiliwa kwa nguvu na wafuasi wa CCM.


Makonda alibainisha kuwa ujio wa Rais Samia utakuwa ni fursa ya pekee ya wananchi wa Arusha kumshukuru kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo barabara, shule, huduma za afya na uwekezaji wa kimkakati unaoendelea mkoani humo.

> “Arusha hii ya leo ni tofauti kabisa na Arusha ya miaka iliyopita. Ni fahari yetu kumkaribisha Mama Samia kwa namna ya heshima na sherehe kubwa, ili aone namna tulivyo pamoja naye,” aliongeza.


Kwa mujibu wa viongozi wa CCM mkoani humo, maandalizi ya mapokezi hayo tayari yamekamilika, huku wananchi wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi kuonyesha mshikamano wao na Rais.





Post a Comment

0 Comments