CRDB YAZINDUA TAWI JIPYA KWA KISHINDO NAMANGA , LITAKUWA KICHOCHEO CHA BIASHARA NA UCHUMI WA WANANCHI MPAKANI -RC MAKALA

Na Joseph Ngilisho– LONGIDO

MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amezindua rasmi Tawi jipya la Benki ya CRDB Namanga, Wilayani Longido, akisema hatua hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha biashara za mpakani na kukuza uchumi wa kikanda.


Akizungumza leo Ijumaa, Septemba 26, 2025, katika hafla ya uzinduzi huo, Makalla alisema tawi la Namanga litakuwa kitovu cha shughuli za kibiashara, kilimo na uwekezaji, na hivyo kuifanya Namanga kuendelea kuwa lango kuu la biashara kati ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya.


> “Serikali pia imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huduma za kibenki za kidijitali, huduma za fedha kupitia simu na uwekezaji kama vile Kijani Bond, Samia Infrastructure Bond na SUKUK ambazo CRDB imekuwa kinara katika kuzianzisha. Huduma hizi za kifedha ni kichocheo muhimu cha ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa,” alisema Makalla.


RC Makalla aliwataka wananchi wa Namanga na Mkoa wa Arusha kwa ujumla kutumia huduma hizo kikamilifu, si tu kwa ajili ya biashara ndogo na kubwa, bali pia kwa kuunganisha huduma za kifedha na sekta ya utalii ili kuhakikisha watalii na wageni wanaofika mkoani humo wanapata huduma za kifedha kwa urahisi.


Aidha, Makalla aliipongeza CRDB Benki kwa kutimiza miaka 30 ya kutoa huduma nchini, akisema uamuzi wa kupeleka huduma mpaka Namanga ni kielelezo cha benki hiyo kugusa maisha ya wananchi katika maeneo yote ya kipaumbele cha kiuchumi.

Akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa CRDB, Bonaventura Paul, alisema tawi la Namanga linaifanya CRDB kufikisha jumla ya matawi 14 mkoani Arusha, kati ya 268 nchi nzima, huku wakiwa na mawakala zaidi ya 1,801 katika Mkoa wa Arusha pekee, na kati ya hao, 120 wapo Wilaya ya Longido.

 


Kwa upande wake, Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Saddat, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini na kuipa nguvu sekta ya kifedha.

> “Tunawahakikishia wananchi wa Namanga na Longido kwa ujumla kuwa sasa huduma zote za CRDB zinapatikana kikamilifu. Tawi hili litakuwa nguzo ya maendeleo ya kifedha na kiuchumi mpakani,” alisema Saddat.

Sauti za Wananchi

Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walieleza kufurahishwa kwao na hatua ya kufunguliwa kwa tawi hilo, wakisema sasa huduma za kibenki zitakuwa karibu na maisha yao ya kila siku.

Neema Saitoti, mfanyabiashara mdogo wa Namanga, alisema:

> “Tulikuwa tunasafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki. Sasa CRDB ipo hapa kwetu, biashara zetu zitakua kwa urahisi.”

Naye Peter  Nnko, mkazi wa Longido, alisema:

> “Namanga ni lango kuu la biashara, tawi hili litasaidia sana wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Hii ni fursa kubwa kwetu wananchi.”


Uzinduzi wa Tawi la CRDB Namanga unatarajiwa kuongeza kasi ya biashara za mpakani, kuongeza ajira, kukuza uwekezaji na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Longido na Mkoa mzima wa Arusha.

Ends..

Post a Comment

0 Comments