RC MAKALLA AKAGUA UJENZI UWANJA WA AFCON ARUSHA

RC MAKALLA AKAGUA UJENZI UWANJA WA AFCON ARUSHA

*Aagiza taasisi za miundombinu kuharakisha huduma muhimu

*Ampongeza Rais Samia kwa Sh. Bilioni 340 za ujenzi

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Gabriel Makalla, leo Ijumaa Septemba 5, 2025, amekagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa utakaotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), unaojengwa katika Kata ya Olmot, jijini Arusha kwa gharama ya Shilingi Bilioni 340.


Ukaguzi huo umefuatia kikao kazi maalum kilichohusisha wakuu wa idara na taasisi za miundombinu ikiwemo TANROAD, TARURA, AUWSA, TANESCO na TTCL. Taasisi hizo zimeagizwa kuunda kikosi kazi maalum kitakachokaa eneo la ujenzi muda wote kwa ajili ya kuratibu na kutekeleza kwa haraka huduma muhimu za maji, umeme, barabara na Mawasiliano.




Akizungumza baada ya ukaguzi huo, RC Makalla alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha hizo, akibainisha kuwa mradi huo utakuwa chachu ya uchumi na maendeleo ya kijamii mkoani Arusha.


“Kama Mkoa wa Arusha tunajivunia utalii. Rais Dkt. Samia ametuletea Royal Tour na sasa anatuletea utalii wa michezo (sports tourism). Uwepo wa uwanja huu utachochea mzunguko wa fedha, kukuza biashara na kuboresha maisha ya wananchi wetu. Tunamuhakikishia Mhe. Rais kuwa tutasimamia ukamilishaji wa uwanja huu kwa wakati ili malengo aliyotarajia yatimie,” alisema Makalla.


Ameongeza kuwa mkandarasi amehakikishia uwanja utakamilika ifikapo Julai 2026, ukizingatia viwango vya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).


Makalla alisisitiza kuwa uwanja huo wa kisasa utatoa heshima kubwa kwa taifa kwani ni mara ya kwanza Tanzania kuandaa AFCON kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.


“Kupitia maamuzi haya ya Rais Samia, Tanzania itapata nafasi ya kipekee ya kushuhudia mashindano makubwa ya kimataifa yakifanyika ndani ya mipaka yake, jambo ambalo halijawahi kutokea,” aliongeza.


Kwa upande wake, Mhandisi Denice Benito Mtemi, mwakilishi wa kampuni ya China Railway Construction inayotekeleza mradi huo, alisema ujenzi umefikia asilimia 60 na tayari mipango ya kuweka nyasi asili katika eneo la kuchezea imeanza.


Alibainisha kuwa kazi inakwenda kwa kasi na kampuni yake imejipanga kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa, ili kuandaa uwanja unaokidhi matarajio ya CAF na wananchi wa Tanzania.

Ends...

Post a Comment

0 Comments