MUNGURE AZINDUA KAMPENI KWA KISHINDO, AAHIDI KUMALIZIA MIRADI YA MAENDELEO AKHERI
Na Joseph Ngilisho – Arumeru
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Akheri wilayani Arumeru kwa tiketi ya CCM, Julias Mungure, ameanza kampeni zake kwa kishindo huku akiahidi kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa barabara, shule na kituo cha afya.
Akihutubia mamia ya wananchi katika uzinduzi wa kampeni hizo ,leo septembe 21,2025 , Mungure alisema tayari kata hiyo imenufaika na Shilingi bilioni 14 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, fedha ambazo zimeelekezwa kwenye miradi mikubwa ya maendeleo.
Miongoni mwa miradi aliyotaja ni pamoja na ujenzi wa barabara tatu kwa kiwango cha lami; Barabara ya Sang’Si hadi Ndoombo, Barabara ya Jeshini na Barabara ya Chuo cha Mifugo. Pia, aliahidi kukamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Maksoro pamoja na Kituo cha Afya Akheri.
Katika sekta ya afya, alisema kata hiyo tayari imepokea Shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya maboresho ya Hospitali ya Wilaya ya Tengeru na inatarajia kupokea Shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto.
Aidha, wananchi wa Akheri wamenufaika na mikopo ya Halmashauri ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu, Shilingi milioni 300 zimetolewa kwa akinamama, vijana na walemavu.
> “Baada ya kukamilika kwa miradi niliyoahidi awali, sitadaiwa mradi wowote. Nitakuwa huru kuanzisha miradi mipya iwapo wananchi watanipa ridhaa ya kuwaongoza tena,” alisema Mungure.
> “Nawaomba mnipatie miezi sita tu nikishaingia bungeni, nitafanya mambo makubwa. Kata ya Akheri ndiyo itakuwa kipaumbele changu kati ya kata zote 26 za jimbo hili,” alisema Nasari huku akiwataka wananchi wasiyumbishwe na madai kuwa hatoshiriki maendeleo ya kata hiyo kwa kuwa ndiyo anayotoka mbunge aliyeondoka.
Awali, akimkabidhi ilani ya CCM kwa mgombea huyo mbele ya waandishi wa habari wa Arushadigital katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Arusha, Flora Zelothe, aliwataka wagombea kuhakikisha wanatekeleza ilani ya chama hicho kikamilifu.
Hata hivyo, Zelothe hakusita kugusia kutokuwepo kwa baadhi ya watia nia waliowania nafasi ya udiwani katika mkutano huo, akidai kitendo hicho kinaonesha kukosa mshikamano wa kichama.
> “CCM ina nafasi nyingi za uongozi. Mtu anayesusa mikutano ya chama hana sababu ya kuomba tena nafasi yoyote,” alisema Zelothe.
Mkutano huo wa kishindo ulijaza mamia ya wananchi na wafuasi wa CCM, hali iliyoashiria mwanzo wa kampeni zenye ushindani mkali katika kata hiyo.
0 Comments